Asema umeakisi dhamira ya ASP

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema ujenzi wa nyumba za mji mpya wa Kwahani, umeakisi dhamira ya Chama cha Afro Shirazi, katika kuwapatia makaazi bora wananchi wa Zanzibar.

Dk. Shein alisema hayo jana katika uzinduzi wa nyumba za mji mpya wa Kwahani, hafla iliyofanyika eneo la Kwahani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka 1961, Chama cha Afro Shirazi kiliazimia kufanya mambo makubwa manne, mambo hayo ni pamoja na kuimarisha afya, elimu, ardhi kuwa mali ya wananchi wote na kujenga makaazi mapya kwa wananchi.

Alisema baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, mzee Abeid Amani Karume alitekeleza azma ya serikali ya kujenga nyumba za maendeleo katika maeneo mbali mbali, ambapo eneo la Kikwajuni likawa la mwanzo katika mwaka 1964, ikifuatiwa na Kilimani, Bambi, Michenzani, Gamba na Makunduchi.

Alieleza katika kuendeleza dhamira hiyo, wazo la kuanza ujenzi katika eneo la Kwahani lilikuja kutokana na mafuriko yanayolikumba eneo kwa nyakati tofauti.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, imebainisha uendelezaji wa ujenzi wa nyumba za kisasa ili kuiwezesha nchi kupiga hatua za maendeleo na kusema miji 14 ya Unguja na Pemba inahusishwa na ujenzi huo.

Alifahamisha kuwa serikali ilifanya uamuzi kuupandisha hadhi Mji wa Zanzibar na kuwa Jiji kamili chini ya kifungu namba 18 cha Sheria namba 7 ya mwaka 2014 ya sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kumteua Mkurugenzi wa Jiji hilo pamoja na Meya, baada ya kukidhi vigezo na mahitaji ya msingi, yakiwemo ya kuwa na Manispaa zaidi ya mbili.

Alisema serikali kwa kushirikiana na ‘Bakhresa Group of Companies’ imefanikiwa kuweka historia kwa kuanzisha mji mpya katika eneo la Fumba na kuweka miundombinu yote muhimu.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Kwahani kwa kukubali kupisha ujenzi wa nyumba hizo na kusema uamuzi wao huo ni wa busara, hivyo akawataka kuzitunza nyumba hizo kwa kufanya matumizi sahihi.