NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema suala la umiliki wa ardhi hapa Zanzibar lilitokana na tamko la marehemu mzee Abeid Amani Karume, katika ‘Manifesto’ ya uchaguzi ya Chama cha ASP mwaka 1963.

Dk. Shein alisema hayo huko Dundua Bumbwini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika ufunguzi wa nyumba za makaazi kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi asilia, hafla ambayo pia ilihusisha uwekaji jiwe la msingi la msikiti na lango la kuingilia bandarini.

Alisema kupitia ilani ya ASP, mzee Karume alitangaza ardhi yote mali ya serikali na kueleza sheria ya ardhi zimebainisha kuwa serikali itachukua eneo lolote la ardhi zinazoendelezwa na wananchi kwa shughuli za maendeleo.

Alisema sheria ya ardhi ya mwaka 1992 imeweka utaratibu wa matumizi na kubainisha Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zenye sheria bora za ardhi barani Afrika.

Alisema serikali itakapoona ipo haja ya kutumia ardhi yake kwa shughuli za maendeleo haitosita kufanya hivyo na kuwalipa fidia wananchi kutokana na rasilimali zilizopo na vipando, jambo ambalo limefanyika huko kijiji cha Dundua.

Aidha, akinasibisha kauli yake na hatua ya wananchi wachache waliopingana na uamuzi wa serikali wa kuondoka katika maeneo yao kupisha ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi asilia, Dk. Shein alisema serikali haiwezi kugombana na wananchi.

Aliwataka wananchi wote waliopata fursa ya kuishi katika nyumba hizo za kisasa kufuata taratibu za ujenzi na kusisitiza umuhimu wa kudumisha usafi ndani na nje ya nyumba hizo pamoja na kuziweka katika mazingira bora.

Akizungumzia sababu ya kuanzishwa ujenzi wa nyumba hizo, alisema unalenga kubadilisha mwelekeo wa uchumi wa Zanzibar kwa serikali kuwekeza nguvu zake katika uchumi wa buluu.

Alisema ili kufikia dhamira hiyo kunahitajika kuwepo miundombinu miwili muhimu, ikiwemo ule wa ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mpigaduri na bandari ya mafuta na gesi asilia katika eneo Mangapwani.

Alisema wakati wa kuanza kwa mradi wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi asilia kulikuwa na watu wenye mitizamo tofauti ikiwemo waliopinga, hata hivyo akabainisha kuwa serikali imetenga eneo la ardhi la kilomita saba kuendeleza mradi huo.

Aliipongeza kamati ya mawaziri wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi kubwa ya kusimamia uendelezaji wa mradi huo pamoja na hatua mbali mbali ilizozichukuwa.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchagua viongozi wenye uwezo, waadlifu, wenye busara na watakaoshirikiana na serikali, katika uchaguzi mkuu baadae mwaka huu, kwa kigezo kuwa ndio watakaofanikisha ujenzi wa bandari hiyo.

Naye, waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib alisema kamati ya mawaziri wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya kazi kwa mashirikiano makubwa ili kuhakikisha kijiji hicho kinajengwa kwa mafanikio.

Alimpongeza Dk. Shein kwa rai yake ya kuwajengea nyumba za makaazi wananchi waliopisha ujenzi huo wa bandari ya mafuta na gesi badala ya kuwakabidhi fedha zao mkononi.

Aidha, alivipongeza vikosi vya KMKM na Mafunzo pamoja na wadau mbali mbali waliojitokeza   kwa kufanya kazi kwa moyo na kufanikisha dhamira na malengo ya serikali.

Mapema, Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Ali Halil Mirza alisema ujenzi wa kijiji kipya cha Dundua uliohusisha nyumba 31 umefanikishwa kwa ushirikiano wa vikosi vya KMKM, Mafunzo na Wakala wa Majengo na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.56.

Alisema ujenzi wa kijiji kipya cha makaazi Dundua ni Utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

Alisema ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi asilia katika eneo hilo utachangia na kuimarisha harakati za kiuchumi pamoja na kuchochea maendeleo.