Asema Dk. Mwinyi mgombea asiye na doa

KHAMISUU ABDALLAH NA MWINYIMVUA NZUKWI

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema wagombea wote walioteuliwa na Chama hicho wana uwezo kuleta mabadiliko ya kiuchumi hapa Zanzibar.

Alisema wagombea hao sio wanagenzi katika medani za siasa na kiutendaji kwani kila kiongozi ana uzoefu katika fani yake na majukumu anayoomba.

Dk. Shein aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya skuli ya Chwaka wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema viongozi hao watapewa ilani ya uchaguzi 2020/2025 ili wasimamie kwa uadilifu utekelezaji wake wa kuwatumikia wananchi bila ubaguzi ikiwa ni dira yake tokea awamu ya kwanza ya serikali zote mbili.

Aliwasisitiza wananchi kumchagua Dk. Hussein Mwinyi ili andeleze mambo mazuri yaliyoanzwa na serikali ya awamu ya saba kwani nafasi hiyo anaiweza na kuimudu kwa uwezo mkubwa.

Aidha Dk. Mwinyi amekutana na makundi mbalimbali katika jamii ambayo yatamsaidia pale atakapoingia madarakani kuendeleza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

“Dk. Mwinyi hajateuliwa na mtu mmoja tumemteuwa watu wengi katika kikao cha kamati maalum na halmashauri kuu na nimkongwe katika siasa ndio tukamchagua na amekubalika ndani ya chama na hata kwa wananchi, kuwa ana uwezo wa kuwaongoza wananchi,” alisema.

Hata hivyo, alibainisha kuwa Dk. Mwinyi ni mtu mwenye nidhamu ya kazi na heshima na chama hakina wasiwasi kwake katika kuwaongoza wananchi.

Aliwaomba wananchi kuwachagua viongozi wote wa CCM kuanzia urais, ubunge, uwakilishi na udiwani ili waendelee kuibadilisha Zanzibar kimaendeleo.

Dk. Shein alibainisha kwamba Jimbo la Chwaka ndio ngome kubwa ya CCM na haijawahi kushindwa katika chaguzi zote zilizofanyika nchini ukiwemo wa mwaka 1961.

“Nataka muendelee kututhibitishia kwa vitendo kuona mnaendeleza heshima yenu msikubali kuwachagua viongozi ambao hawana maslahi na taifa letu,” aliwasisitiza.

Akiomba kura kwa wananchi wa wilaya ya kati mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi alisema endapo atapata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar atahakikisha anaimaliza ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Binguni.

Alisema, serikali ya awamu ya saba imeimarisha sekta ya afya kwa asilimia kubwa ikiwemo kupandisha hadhi vituo vya afya vilivyokuwemo katika mkoa huo ili wananchi wapate huduma bora na kuepusha kufuata huduma hizo maeneo ya mbali. 

Sambamba na hayo, aliahidi kumaliza kero ya upatikaji wa maji safi na salama katika baadhi ya maeneo katika kijiji cha Jumbi, Unguja Ukuu na Chwaka, ujenzi wa barabara za ndani na kuimarisha kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa lengo la kupata mavuno mengi ya chakula.

Mbali na hayo Dk. Mwinyi, aliahidi kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji kwa kuweka mipango mizuri ya ardhi ili kuondoa migogoro hiyo.

Katika kuimarisha zao la ndimu katika kijiji hicho Dk. Mwinyi aliahidi kujenga Viwanda vya kusarifu zao hilo sambamba na kuweka doria katika bahari ili kudhibiti uvuvi haramu katika ukanda wa bahari.

Aliwasisitiza wananchi kutokubali kuubeza muungano wao kwani una manufaa makubwa kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Hivyo aliwaomba waananchi kumchagua na kuwachagua viongozi wote wa CCM ili waweze kushirikiana katika kuleta maendeleo.

Aliipongeza serikali ya awamu ya saba kwa mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa skuli za horofa katika kijiji cha Uroa na Binguni.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Ramadhan Abdalla Ali alisema CCM imejipanga kuhakikisha inashinda na utekelezaji wa hilo ni Oktoba 28 mwaka huu katika visanduku vya kura.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Sadala alisema CCM itaendelea na kampeni zake za mtaa kwa mtaa na viwanja kwa vijana ili kuomba ridhaa kwa wananchi kwa kuona wananchi wanaendelea kuiamini CCM katika kuwaletea maendeleo.