NA MWINYIMVUA NZUKWI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa barabara ya Fuoni – Kombeni utakaofanyika katika viwanja vya hospitali ya Kombeni, wilaya ya Magharibi ‘B’, Unguja.

Ofisa habari wa wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nafisa Madai Ali alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 8.5 ni miongoni mwa barabara zilizopangwa kujengwa na serikali ikiwemo ya Bububu – Mahonda – Mkokotoni iliyofunguliwa mapema mwaka huu.

Alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umetekelezwa na kampuni ya CCECC ya China ambayo pia ilijenga barabara ya Bububu – Mahonda – Mkokotoni, umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.1 chini ya usimamizi wa kampuni ya H. P. Gauff ya Ujerumani.

“Barabara hii itakumbukwa ni miongoni mwa barabara ambazo kampuni ya CCECC ya China ilikubaliana na serikali kuijenga, hivyo baada ya kukamilika tunaamini itapunguza changamoto ya usafiri kwa watu wa wilaya ya Magharibi ‘B’ ambao wataweza kuunganika na wa wilaya ya Kusini bila ya kuja mjini,” alisema ofisa huyo.

Mbali na Dk. Shein, ofisa huyo alisema viongozi mbali mbali wa serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi wa maeneo ya ndani na nje ya wilaya hiyo wanatarajiwa kuhudhuria kushuhudia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2015/2020.

Barabara nyengine zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni Matemwe – Mbuyu, Pale – Kiongele na nyongeza za kipande cha Bububu Polisi hadi Bububu kwa Nyanya ambazo zote zina urefu wa kilomita 54.8.