Azindua barabara mbili mpya

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya miundombinu ni kielelezo cha kuyaendeleza mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Dk. Shein alieleza hayo jana huko Kombeni wakati akiwahutubia wananchi katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Kombeni hadi Fuoni iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa barabara ya Koani hadi Jumbi.

Alisema mapinduzi ndiyo yaliyokomboa kila kitu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwani kila kitu cha maendeleo katika visiwa vya Unguja na Pemba chanzo chake kinatokana na mapinduzi ya mwaka 1964.

Alifahamisha kuwa ujenzi wa barabara hizo ni miongoni mwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kwamba zitakuwa kiungo kikubwa cha harakati za usafiri wa kujiletea maendeleo kwa wananchi.

Dk. Shein amesema shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zinategemea miundombinu ya barabara zilizo bora pia, juhudi za kuimarisha kilimo, utalii, uwezeshaji na za kiuchumi zinahitaji uwepo wa barabara za kisasa.

Aliongeza kuwa kuimarika kwa miundombinu ya barabara ndio chachu ya maendeleo na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuimarisha miundombinu ya barabara ili itoe msukumo katika jitihada za kuendeleza sekta nyengine.

“Nimefarajika tumefanikisha kumalizika ujenzi wa barabara hizi tatu nilizoahidi kuzimaliza kabla ya muda wangu wa uongozi”,alisema Dk. Shein akielezea barabara za Fuoni-Kombeni, Koani-Jumbi kwa Unguja na Ole-Kengeja kwa Pemba.