NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAKAMU wa Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amewaeleza wananchi wa Micheweni kwamba dawa ya viongozi wanaohubiri chuki ni kuwanyima kura na badala yake kura hizo kukipigia Chama cha Mapinduzi.

Dk. Shein alieleza hayo katika uwanja wa Shaame Matta huko kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi na wagombea wengine wa nafasi mbali mbali.

Alisema dawa ya kuwakataa viongozi wa namna hiyo na kutowapigia kura na kwamba kura zote kipigie chama cha CCM, ambacho kina thamini misingi ya utu na heshima ya kila mwananchi.

Alisema chama hicho tawala ndicho chama kilichoikomboa nchi kwamba mapinduzi ya 1964, ndiyo yanayomfanya kila mwananchi atembee kifua mbele, na ili kukipa tuzo chama hicho ni kukurejesha tena madarakani.

Alisema tayari ilani ya CCM ibainisha kuyalinda mapinduzi hayo yenye lengo la maendeleo kwa wote na ameshakabidhiwa mgombea urais wa Zanzibar wa chama hicho ili ayaendeleze.

“Mapinduzi yetu ndio maendeleo yetu, iwe upatikanaji wa huduma ya maji safi, elimu bure, barabara na hata hapa Micheweni panang’ara kwa maendeleo yaliyotokana na mapinduzi”, alieleza.

Akimuelezea mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM, ambae ni rais wa Zanzibar alisema, Dk. Mwinyi ana sifa za kuwa rais wa Zanzibar.

Alisema Dk. Mwinyi ni mchapa kazi asiyechoka kutokana na utendaji wake wa kazi uliotukuka, hivyo kwa Zanzibar hakuna mbadala wake kutoka kwa wagombea wa vyama vyengine.

Alisema, Dk. Mwinyi kisiasa ameshahudumu nafasi kadhaa ikiwa pamoja na mjumbe wa kamati kuu, waziri wa Ulinzi na ndio maana, sifa anazozitaja anazo kwa dhati.

Alieleza kuwa, Dk. Mwinyi ana nia ya kweli ya kuwatumikia watu wote tena bila ya ubaguzi na kilichobakia kwa wananchi wa Micheweni na maeneo mengine yote ya Zanzibar ni kumpigia kura za ndio mgombea huyo.

Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Dk. Shein alisema, umedumu kwa miaka 56 bila ya kutetereka, tofauti na nchi nyengine kama vile Senegal na Gambia na ule wa Misri na Libya ambazo zilishindwa.

Aidha, aliwaomba wanachama wa vyama vyengine kuhakikisha wanawapigia kura wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi madiwani.

Kwa upande wake mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi, alisema iwapo atapata ridhaa atahakikisha anainua uchumi kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema dhamira yake ya kuomba nafasi hiyo, ni kutaka kuwatumikia kwa dhati wananchi wote tena bila ya ubaguzi, ili kuona kila mmoja, anajiweza kiuchumi.

Alisema, kutokana na Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 ilivyotekelezwa vyema kwenye maeneo kadhaa ya huduma za kijamii, kazi yake ni ndogo katika maeneo yaliobakia.