NA HAFSA GOLO

HALMASHAURI ya Kaskazini “A” Unguja imesema katika msimu huu wa kilimo cha mpunga jumla ya ekari 1,500 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya upandaji wa zao hilo ambapo ekari 300 zitakuwa za umwagiliaji maji.

Msaidizi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ngwali Makame Haji, alisema  hayo wakati akizungumza na gazeti hili katika  muendelezo wa ziara maalumu ya kusikiliza kero za wakulima na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa kilimo hicho katika msimu huu iliyofanyika Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.

Alisema lengo la kukaa pamoja na wakulima wa zao hilo ni kuhakikisha ekari hizo zinalimwa na kupandwa kwa wakati unaostahiki, ili kuleta mafanikio kwa wakulima na taifa kwa jumla.

Ngwali alisema, iwapo halmashauri zitasimamia ipasavyo utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima wa zao hilo na mazao mengine upo uwezekano mkubwa Zanzibar kuendelea kuondokana na uhaba wa chakula sambamba na wakulima kufikia malengo waliojiwekea.

” Moja ya eneo  muhimu linalopaswa kupewa kipaombele na halmashauri zetu ni kuhakikisha wakulima wote  wanapata nyezo na pembejeo za kilimo kwa wakati, ili waweze kuwajibika vyema na kupata  mavuno mazuri”,alisema.