ANKARA,UTURUKI
RAIS wa Uturuki Rwecep Tayyip Erdogan ametoa hasira yake kuhusu kibonzo alichosema kinachukiza jarida la tashtiti la Kifaransa linalochapishwa kila wiki la Charlie Hebdo kikimuonesha akiwa ameishika sketi ya mwanamke huku akinywa bia wakati amevaa nguo za ndani.
Ofisi ya Erdogan iliapa kuchukua hatua ya kisheria na kidiplomasia wakati televisheni ya Uturuki ya NTV ilisema serikali pia ilimuita naibu balozi wa Ufaransa kulaani tukio hilo.
Ufaransa ilimuita mjini Paris balozi wake wa Uturuki kwa ajili ya mashauriano katika ishara zaidi ya kuzorota mahusiano ya kidiplomasia kati ya washirika hao wawili wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Katuni hiyo ya ukurasa wa mbele wa jarida la Charlie Hebdo ilikuja siku kadhaa baada ya Erdogan kutoa wito wa kususia bidhaa za Ufaransa na kuhoji hali ya kiakili ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kuchochea hisia dhidi ya Uislamu.
Kulishuhudiwa maandamano ya hasira kote Uturuki na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu kupinga matamshi ya Macron.