MOSCOW, URUSI

UMOJA wa Ulaya umemuwekea vikwazo bilionea wa Urusi, ambaye ni mshirika mkuu wa Rais Vladimir Putin, anaetuhumiwa kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani, kusaidia kuhujumu usalama wa Libya, na kuvunja vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa, juu ya kuliuzia silaha taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Taarifa ya Umoja wa Ulaya inasema kuwa, umoja huo unaweka vikwazo vya kusafiri na kuzuwia mali za Yevgeny Prigozhin, kwa kile kinachosemekana ni kushiriki kwake kwenye kutoa msaada, na kujihusisha na kuchafua amani, usalama na utulivu wa Libya.

Taarifa hiyo inasema kuwa, mfanyabiashara huyo wa Kirusi, ana mafungamano makubwa, yakiwemo ya kifedha, na kampuni ya kibinafsi ya kijeshi ‘Wagner Group’ inayoendesha shughuli zake nchini Libya.

Bilionea huyo pia, ni mmoja kati ya Warusi kadhaa waliotiwa hatiani nchini Marekani, kufuatia uchunguzi wa Robert Mueller, kwa kufadhili udukuzi wa mitandaoni, uliouchafuwa uchaguzi wa 2016.