MWANTANGA AME

LEO ni Oktoba 14, ikiwa ni miaka 21 sasa tangu Rais wa kwanza wa Tanzania na baba wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere kufariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, mjini London, Uingereza.

Yeye alikuwa miongoni mwa viongozi wa Kiafrika walioshiriki moja kwa moja katika vita vya ukombozi wa bara hilo hasa za Kusini mwa Afrika pale nchi hizo zilipokuwa zikisaka uhuru.

Licha ya kwamba marehemu Julius Nyerere, amefariki na kuyaacha mengi ya kumbukumbu ambayo yanatumiwa na kizazi cha sasa  kutokana na mafundisho ya juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ikiwa ni sera yake aliyoitumia kwa watanzania na kuwaunganisha kuwa wamoja.

Lakini  sasa sera hiyo haitekelezwi, kinyume na ilivyokuwa pale alipokuwa madarakani, hata hivyo Watanzania wanapobishana katika masuala mbali mbali hurejea nyuma na kumkumbuka Mwalimu Nyerere kama kituo cha uadilifu.

Sambamba na hilo pia Mwalimu anasifiwa kuwa muasisi wa Muungano wa Tanganyika na Visiwa vya Zanzibar, pale alipokubaliana na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na kupelekea nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania taifa ambalo mpaka sasa limedumu katika miaka 56 tangu kuasisiwa kwake.

Alikuwa mkakamavu juu ya Muungano huo na kuyapuuza matakwa ya baadhi ya watu waliotaka kujigawa na kuwa sehemu mbili za Muungano iwapo wangefanikiwa, jambo ambalo daima hakulitaka.

Aidha Hayati Mwalimu Nyerere pumzi zake pia alilielekeza Bara la Afrika kuwa na Umoja, mfano wa Umoja wa Ulaya ulimvutia jambo ambalo alifanikiwa kwani amefariki kwa kuiacha Tanzania ikiwa na umoja wa Nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC)

Mwalimu Nyerere, jambo jengine ambalo alikuwa akilihubiri sana ni suala la ukabila, jambo ambalo hadi sasa halina nafasi katika mukhtaza wa Tanzania ya leo.

Mambo mengine ambayo aliyasimamia ni suala la kupinga Udini ni jambo ambalo alisisiza sana katika hotuba zake, hasa kuwaasa viongozi wasitafute uongozi kwa kutumia dini, kwa kuona mambo haya ya yanachochea chuki za dini yakianza na wakiyapa nafasi hayana sumile.

Aidha sera yake ya kufuta ujinga, maradhi na Umaskini, ndiye iliyochangia kufikia Tanzania yenye maendeleo makubwa jambo ambalo ni la kujivunia.