KAMPALA,UGANDA

OFISA wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), katika eneo la Afrika Mashariki  Cyril Ferrand, amesema kanda ya Pembe ya Afrika inaweza kukabiliwa na wimbi jipya la nzige wa jangwani kama hatua hazitachukuliwa kupunguza hali hiyo .

Ferrand alisema wadudu hao ambao wamekuwa wakiongezeka kutokana na hali nzuri ya hewa, wanaweza kuvamia maeneo makubwa ya Pembe ya Afrika.

Alieleza kuwa upepo mkali unavuma kutoka sehemu ya kaskazini na kuelekea kusini, na kurudisha nzige wa jangwani katikati ya eneo la kusini mwa Ethiopia na Somalia, na pia unaweza kuwapeleka Kenya mwishoni mwa Desemba au mapema zaidi.

Alisema huenda nzige hao hawatosababisha msukosuko mkubwa wa kibinadamu katika kanda hiyo ikilinganishwa na mwaka jana kutokana na hatua kali za ufuatiliaji na udhibiti.

Hata hivyo alisisitiza kuwa ni lazima kufuatilia vizuri kizazi kipya cha nzige, na kuchukua hatua za kukabiliana nao haraka iwezekanavyo.