WASHINGTON,MAREKANI

SHIRIKA la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani, FDA limeelezea kiundani mahitaji wanayopaswa kuzingatia waendelezaji wa chanjo za virusi vya corona wanaolitaka liidhinishe matumizi ya dharura ya chanjo zao.

Shirika hilo lilitoa miongozo inayotakiwa kufuatwa na kampuni za utengenezaji dawa iwapo zitataka kuomba idhini ya dharura kwa chanjo zao kabla ya kukamilika kwa majaribio ya kitabibu.

Miongozo hiyo inasema kuwe na walau miezi miwili ya ufuatiliaji baada ya washiriki wa utafiti kupokea chanjo,kutathmini miitikio ya kinga maradhi yao na matokeo mengine.

Miongozo hiyo pia inajumuisha data salama za watumiaji zaidi ya 3,000 wa chanjo hizo zinazoonyesha athari kwenye afya zao.

Mahitaji hayo yanaonekana kuwa ni magumu vya kutosha kufanya matumizi ya dharura ya chanjo hizo nchini humo kabla ya uchaguzi wa urais mwezi Novemba karibu yasiwezekane.

Baadhi ya wataalamu wanasema wanakubali ukweli kwamba miongozo hiyo itahakikisha kwa kiasi fulani chanjo hiyo ni salama,lakini wengine wanasema masharti magumu zaidi yanapaswa kuwekwa kwa matumizi ya dharura ya chanjo.