NA SAIDA ISSA, DODOMA 

JESHI la Polisi Mkoa  wa Dodoma linamshikilia fundi ujenzi Daniel Masawe(40) maarufu kama Madevu mkazi wa Kisasa Medeli kata ya Makulu  kwa kumjeruhi binti kwa risasi, sababu  ikitajwa ni ugomvi wa kimapenzi.

Binti huyo ambaye hakutajwa kwa sababu za kiupelelezi amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Dodoma akiendelea na matibabu.

Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa na Bastola aina ya BROWING CALB 7.65 A748082 CAR NO.95632 ikiwa na risasi saba .

“Tulimkamata akiwa na risasi saba baada ya kupewa taarifa kuwa amemjeruhi binti huyo kwa kutumia risasi kinyume cha sheria na kuhatarisha maisha ya watu wengine”alisema

Aidha kamanda Muroto alisema pia limewatia mkononi watuhumiwa watatu wakiwa na silaha ya kivita ya aina ya AK 47 yenye namba UR2716 ikiwa na risasi zake 27 ambayo wanaitumia katika uhalifu wa ujangili.

Alisema watuhumiwa hao wanajishughulisha na kilimo, lakini pia hufanya ujangili na wanatambulika kwa majina yao ambao ni  ni Juma    Mngoya (40), Amrani Mohamed(34) na Furaha Masaka

“Tumewakamata wakiwa na silaha ambayo inatumika vitani lakini wao wanatumia kufanya ujangili na sasa tumewatia mkononi na tutawapeleka mahakani ili tujiridhishe kuwa watuhumiwa walikuwa wanafanya uhalifu wa aina gani,”alieleza.

Kamanda Muroto, alisema jeshi la polisi linawashikilia watuhumiwa wanne kutoka Mpwapwa na Kondoa mkoani Dodoma kwa kukutwa na meno ya Tembo.

Alisema linamshiukilia Nzara Simony (21) Mkazi wa Kijiji cha Ikengwa Kata ya Kinyasi Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma,  akiwa na meno mawili ya tembo kinyume na sheria.

Alitaja kuwa watuhumiwa wengine ni kutoka wilaya ya Mpwapwa ambao ni  Nchemba Masonga(75), Simon Kitereja(38) na Daud Nhimko(48 ) watuhumiwa wote walikutwa na meno ya tembo ambayo ni kunyume na sheria.