NA KHADIJA KHAMIS, MAELEZO ZANZIBAR

 MKURUGENZI Operesheni na Huduma za Kibinaadam wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Haji Faki Hamdani, amesema eneo la Fungurefu ambako wafanyabiashara wa dagaa wameweka makaazi haliko katika mazingira mazuri na kunaviashiria vya kutokea maafa. 

Aliyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo hilo lililopo Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja na kueleza kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu wanaofika eneo la fungurefu hasa kipindi cha  msimu wa dagaa na upungufu wa huduma ya vyoo kunahatarisha usalama wa afya za wananchi hao. 

Alisema zaidi ya watu 3,000 hukaa katika eneo hilo huku majengo ya vyoo ni manne na kila moja linamatundu 12, hali  inayoonyesha uhaba mkubwa wa vyoo uliopo katika eneo hilo.

Aidha alisema kutokana na upungufu uliopo wa vyoo, imebainika baadhi ya watu hujisaidia sehemu zisizo rasmi na kunaweza kuwa chanzo cha kutokea maradhi ya mripuka. 

Nae Mkuu wa Divisheni ya Operesheni na Huduma za Kibinaadamu kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Jabu Sharif Haji, alisema  wafanyabiashara wa diko  la fungu refu wako katika usalama mdogo kulingana na kutokuwepo na huduma bora za kijamii. 

Alifahamisha kuwa ukosefu wa huduma muhimu katika eneo hilo kutasababisha  viashiria vya janga linaloweza kusababisha maafa, hivyo alilitaka Baraza la Mji Kaskazini ‘A’ kuwawekea huduma  hizo . 

 Aidha, alieleza kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama kwa wakaazi hao huwa ni chanzo cha visababishi vya maradhi ya matumbo na  eneo hilo kwa sasa tayari ni kijiji kutokana na kuishi kwa watu wengi hivyo ni vyema mamlaka husika kuwasogezea huduma za afya katika eneo hilo.

Mkuu wa Diko  la Fungu refu, ambae pia ni  Mfanyakazi wa Baraza la Mji Kaskazini ‘A’ , Kaite Mwadini Haji, alikiri kuwepo kwa kadhia hiyo na kuiyomba mamlaka husika  kuwafikiria huduma muhimu ili waepukane na viashiria vya maafa. 

Hata hivyo, wameiomba Serikali kuwasogezea huduma ya Kituo cha Polisi,  kwani kuna baadhi ya wageni kutoka nje ya mji huvamia bila ya kujulikana taarifa zao, kwa vile wanapokea watu mbali mbali kutoka nje ya mji wakiwemo kutoka Kipumbwe, Mkuja Tanga na Wakongo hufika hapo kufanya biashara za madagaa.

 ” Tunapokea Wageni mbalimbali  kutoka Kipumbwe, Mkuja Tanga pamoja na Wakongo huja na wenyeji wao   Wageni wanaofika hapo wanaletwa na wenyeji wao ,wanaoingia  kiholela hukamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi kwa uchunguzi zaidi.”alisema Mkuu huyo.