NA LAYLAT KHALFAN

ALIEENDESHA gari ikiwa haina mtungi wa kuzimia moto    amefikishwa katika mahakama ya Mwanzo Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo ni Mambo Mgeni Mambo (43) mkaazi wa Melinne Unguja, alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Amina Mohamed Hakimu na kusomewa shitaka lake na Mwendesha mashitaka Kombo Rajab.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo akiwa dereva wa gari yenye namba za usajili Z 479 FK, inayokwenda njia 339 akitokea upande wa Mkunazini kuelekea Mnazimmoja ambapo alipatikana akiendesha gari hiyo ikiwa haina mtungi wa kuzimia moto, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aidha ilibainika kuwa, kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 50 (1)(A) na Kinyume na kifungu cha 58 kanuni ndogo za magari ya biashara ya mwaka 2005, chini ya Kifungu cha 80 sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Oktoba 14 mwaka huu, majira ya saa 4:10 asubuhi huko Benmbela Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Aliposomewa shitaka lake hilo mshitakiwa huyo, alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe ombi ambalo halilikubaliwa mahakamani hapo.

Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 20,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wawiki mbili.

Mshitakiwa  alilipa faini hiyo, ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo kama alivyo amriwa na Hakimu Nassim.