NAIROBI,KENYA
POLISI nchini Kenya wamethibitisha kwamba watu wawili wamefariki katika makabiliano kati ya wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.
Ruto, ambaye alikuwa anahudhuria ibada ya kanisa katika eneo la Murang’a, ngome ya rais Kenyatta iliopo eneo la kati Kenya, alilaani tukio hilo lililowalazimu polisi kurusha vitoa machozi ndani ya kanisa kuwatawanya vijana waliokuwa wakishambuliana kwa mawe , kuchoma magurudumu ya magari na kufunga barabara kuu.
Rais Kenyatta ambaye yuko Ufaransa kwa ziara ya kikazi na Ruto walitofautiana katika hatua ambayo iliwafanya maofisa wa chama tawala Jubilee kupendekeza naibu wa rais kuondolewa kama naibu kiongozi wa chama hicho kilichobuniwa mwaka 2012.
Ruto anapania kumrithi Kenyatta kama rais mwaka 2022 lakini anakabiliwa na upinzani kutoka kwa wafuasi wa Kenyatta wanaodai kuwa alianza kufanya kampeni mapema miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu.
Wawili hao waliingia madarakani wakiahidi kuunganisha taifa na kukomesha migawanyiko ya kisiasa lakini Serikali yao ililaumiwa kwa kuzidisha migawanyiko ya kikabila na ufisadi ambao ulisababisha nchi kupoteza mamilioni ya dola ikiwemo dola milioni 7.8 za kununua vifaa vya kukabiliana na Covid 19, ambayo sasa inaasadikiwa huenda zimeibiwa.
Uchunguzi wa awali na ripoti za Tume ya kukabiliana na ufisadi, Kamati ya bunge la Seneti na ya ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu nchini Kenya zilifichua kuwa wanasiasa na wafanyabishara ambao ni wandani wa mirengo yote miwili ya chama tawala walihusika na ufujaji wa raslimali za umma.