Zaspoti
BENCHI la ufundi la timu ya Gulioni FC, limesema wapo katika mchakato wa kucheza mechi ya kirafiki na Simba baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Gulioni FC ilifanikiwa kupanda daraja la kwanza kanda ya Unguja katika msimu uliomalizika.
Akizungumza na gazeti hili, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Burhan Himid Msoma, alisema, hiyo itakuwa ni miongoni mwa hatua za maandalizi ya kujiandaa na ligi hiyo huku wakiamini itakuwa njia kubwa ya kuwapima wachezaji wake.


Alisema matarajio yao makubwa mechi hiyo itapigwa huko jijini Dar es Salaam.
Alisema mbali na mechi hiyo wanatarajia kucheza mechi nyengine nne na timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, ikiwemo KMKM, KVZ, Mlandege pamoja na Malindi SC.
“Hizo ndizo timu ambazo nastahaki kucheza nazo kwa kiwango cha wachezaji wangu naamini hapo nitajifunza mengi”, alisema.


Alisema malengo yake ni kupambana kuhakikisha anaindaa timu hiyo kwa kila hali ili kifanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Zanzibar msimu ujao.
“Nitakapokamilisha malengo yangu haya kuipandisha tena daraja timu yangu naamini nitakuwa kocha nzuri zaidi maana miaka miwili niliokuwa nayo timu hiyo tayari nimeshaipatia makombe matatu tofauti na kuipandisha daraja”, alisema.


Aidha alisema baada ya kuona mapungufu amelazimika kuongeza wachezaji watano, nafasi ya washambuliaji watatu na viungo wa kati wawili.
“Hizo ndizo nafasi zenye upungufu kwenye timu yangu na tayari nishazifanyia marekebisho mapema”.
Alisema baada ya kupata mapumziko mafupi tayari ameanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo.
Gulioni FC itaungana na timu ya Uhamiaji, Idumu, Kilimani City,Ngome,Taifa Jang’ombe, Jango’mbe Boys, Dulla Boys, Mwembe Makumbi, Mchangani United na Mchangani Star kucheza ligi hiyo msimu wa mwaka 2020-2021.