NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya wilaya Mwanakwerekwe imeiahirisha kesi inayomkabili Ashura Othman Sultan (42) mkaazi wa Jang’ombe hadi Novemba 16, mwaka huu, kwa ajili ya kusikiliza ushahidi.

Hakimu mdhamini wa mahakama hiyo, Mohammed Subeit, aliiahirisha kesi hiyo baada ya ombi lilotolewa na upande wa mashitaka kuomba kuhairishwa kesi hiyo kutokana na kutopokea shahidi.

Kesi hiyo, ilifikishwa mahakamani hapo Oktoba 13, mwaka huu, kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi lakini Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Simni Mohammed alidai kuwa hajapokea shahidi na kuomba kuhairishwa na kupangiwa tarehe nyengine.

Hakimu Subeit, alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 16, mwaka huu, na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kupatikana na chupa moja ya plastik lita moja na nusu na madumu matano yenye ujazo wa lita 20 yote yakiwa na pombe ya kienyeji kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alitenda tukio hilo Mei 28, mwaka 2018, majira ya saa 6:30 mchana huko, Jang’ombe wilaya ya mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kosa la kupatikana na pombe ya kienyeji ni kiyume na kifungu cha 3 (a) sura ya 164 sheria za Zanzibar kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 5 (a) (b) cha sheria namba 10 ya mwaka 1971 sheria za Zanzibar.