NA KHAMISUU ABDALLAH

TUME ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), imesema haijapokea taarifa rasmi kwa mgombea yoyote wa kiti cha urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliyejitoa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Imesema kutofanya kampeni kwa baadhi ya wagombea hao haiondoi sifa ya kuwa mgombea katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 nchini Tanzania.

Kamishna wa Tume hiyo, Hasina Omar, aliyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika kituo cha Uangalizi habari na matokeo cha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Maruhubi na alisema NEC imepitisha wagombea 17 kati ya wagombea 19 walioomba kuteuliwa nafasi hiyo.

Alisema vyama vilivyoteuliwa ni pamoja na AAFP, ACT wazalendo, Ada Tadea, ADC, Chama cha Mapinduzi,CCK,Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Chaumma, Chama cha Wananchi CUF, DP, Demokrasia Makini, NRA, NCCR Mageuzi, Sau, UMD na UPDP.

Hata hivyo, alibainisha kwamba NEC imeteua wagombea wa kiti cha urais na Makamo wa Rais kutoka vyama 15 vya siasa ambapo katika uteuzi huo wanawake wawili walijitokeza na kuteuliwa kugombea kiti cha Rais na wanawake watano walijitokeza na kuteuliwa kugombea nafasi ya Makamu wa Rais.

Alisema kutokana na hali hiyo NEC imepitisha wagombea wote na watakuwemo katika karatasi ya kupigia kura siku ya uchaguzi.

Alibainisha kwamba ni mara ya kwanza kwa Tanzania vyama vingi vya siasa kusimamisha wagombea wa kiti cha urais hali ambayo inaashiria kukuwa kwa demokrasia nchini.

Hivyo, aliahidi kuwa tume imejipanga vizuri kuona vifaa vinasambazwa kwa wakati vituoni na kuhakikisha kila mwenye sifa anapata haki yake ya kupiga kura kwa mujibu wa katiba.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi upande wa Zanzibar, Hamidu Mwanga, alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 74 (6) tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na wabunge wa Tanzania na madiwani kwa bara.

Hivyo, aliwahakikishia wananchi kuwa NEC itahakikisha inasimamia uchaguzi huo kwa kufuata katiba, sheria na miongozo ili kuona uchaguzi unakuwa wa uwazi, huru na haki.

Akizungumzia utoaji wa matokeo siku ya uchaguzi alisema ni kosa la jinai kwa mgombea yoyote kutangaza matokeo na kazi hiyo inafanywa na tume pekee hivyo aliwasisitiza wagombea kujiepusha na kosa hilo.