BERLIN,UJERUMANI

MJI wa mashariki mwa Ujerumani wa Halle unafanya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutokea shambulizi la kigaidi lililofanywa na mtu wa siasa kali za mrengo wa kulia kwenye hekalu la mjini humo wakati wa siku kuu ya Kiyahudi ya Yom Kippur.

Mkuu wa shirika la usalama wa ndani la Ujerumani BfV, Thomas Haldenwang, alionya kuwa Ujerumani inashuhudia ongezeko la vitendo vya chuki dhidi ya Mayahudi.

Akizungumza na gazeti la Taggesspiegel, Haldenwang alisema katika miaka miwili iliyopita, makosa ya uhalifu, yakiwemo matukio ya mashambulizi dhidi ya Mayahudi na taasisi za Kiyahudi nchini Ujerumani yaliongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mnamo Oktoba 9, 2019 mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 27 alijaribu kuingia kwa nguvu kwenye hekalu hilo kwa kufyatua risasi mlangoni bila kufanikiwa na badala yake akawauwa watu wawili waliokuwa nje kabla ya kutoroka na kisha kukamatwa.