NAIROBI, Kenya

TIMU ya taifa ya Kenya Harambee stars imepanda kwa nafasi tatu zaidi kutoka nambari 106 hadi 103, kwenye orodha ya viwango bora vya kimataifa iliyotolewa  na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kupanda ngazi za Stars kumechangiwa na ushindi wa 2-1 kwenye mchuano wa kirafiki uliowakutanisha na Chipolopolo ya Zambia Oktoba 9, 2020, uwanjani Nyayo, Nairobi.

Ni mara ya pili mfululizo kwa Stars kupanda ngazi kwenye msimamo wa FIFA baada ya kuorodheshwa ya 106 kutoka 107 mnamo Septemba 17, 2020.

 Kenya wamepangiwa kuvaana na viongozi wa Kundi G, Comoro kwenye mechi mbili zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON), chini ya kocha mpya, Jacob ‘Ghost’ Mulee aliyerithi mikoba ambayo Francis Kimanzi aliyepokonywa nafasi hiyo na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wiki hii.