PARIS,UFARANSA

UFARANSA inakabiliwa na ukosoaji unaozidi kuongezeka kutoka kwa Waislamu kufuatia maoni ya Rais Emmanuel Macron kuhusiana na vibonzo vya Mtume Muhammad.

Macron aliahidi kulinda uhuru wa kujieleza baada ya mwalimu aliyewaonyesha wanafunzi vibonzo vya Mtume huyo kuuawa mapema mwezi huu.

Macron alisema hataondoa haki ya umma kuonyesha vibonzo.

Maoni yake yalichochea miito ya kususia bidhaa za Ufaransa na maandamano,kwani Waislamu wanachukulia kuwa ni kukufuru kusawiri picha za Mtume.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alitoa wito wa kusitishwa kwa kampeni ya chuki dhidi ya Waislamu inayoongozwa na rais wa Ufaransa.

Erdogan aliwataka Waturuki kutonunua bidhaa za Ufaransa.

Maandamano yalizuka nje ya ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Washiriki walizichoma bendera za Ufaransa na picha za Macron.

Miito ya kususia bidhaa pia inaongezeka miongoni mwa Waislamu mitandaoni.