NA ABOUD MAHMOUD

SOKO lililoanzishwa karibuni hapo Kijangwani, mjini Unguja,  ambapo awali lilitarajiwa kuwa kituo kikuu cha gari za dala dala zinazotoa huduma katika mji wa Zanzibar na maeneo ya karibu imezusha adha kubwa kwa watu wa maeneo ya karibu.

Hii inatokana na baadhi ya wafanya biashara wa soko hilo kuharibu mazingira kwa kuchafua vichochoro vya sehemu hio kwa kujisaidia na kutupa chupa zenye mikojo badala ya kutumia vyoo viliopo ndani ya soko hilo.  

Hivi karibuni kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ilitoa taarifa yenye kusikitisha na kukirihisha  kwa wakaazi wa maeneo ya Mwembeladu karibu na kituo cha gari za abiria zinazokwenda mashamba na madereva, utingo  na wafanya biashara wa pembezoni mwa hilo soko.

Katika malalamiko hayo watu mbali mbali walielezea namna uchafu ulivyokithiri hapo mtaani .

Hali hii inahatarisha maisha ya watu wanaoishi karibu na hilo soko na pia kuwaweka watoto wadogo katika hali ya hatari kwa vile katika michezo yao wanaziokota hizo chupa za mikojo au hata kuchezea mifuko yenye kinyesi.

Kilio cha wananchi hao ni cha kuhuzunisha kwani kitendo cha watu wazima na wenye akili timamu kutumia chochoro za nyumba hizo na kuzifanya vyoo ni jambo la hatari sana na linaweza kusababisha miripuko ya maradhi mbali mbali.

Wananchi hao walisema vitendo hivyo hufanywa na wafanyabiashara wa maeneo hayo  na utingo na madereva wa gari za shamba wanaotumia chupa za maji kufanya haja ndogo na baadaye kuzitupa katika maeneo hayo.

Baya zaidi ni kwamba tatizo hilo pia lipo katika maeneo ya hospitali ya wazazi ya Mwembeladu ambapo mwandishi alizungumza na wafanyakazi na wananchi wanaoishi maeneo hayo ya karibu na kusikia kilio chao.

Wengi wao wamesema kwamba ukosefu wa vyoo karibu na kituo cha magari ya shamba kumezidisha kuifanya hali kuwa mbaya na ya kutisha.

Kwa kutilia maanani kwamba hali ya uchafu kama huu unaoonekana sehemu hio kumesababisha maradhi ya miripuko siku za nyuma ni vyema hali hii ikazingatiwa kwa umuhimu mkubwa na hatimaye kufanywa juhudi za haraka ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili.

Kuvigeuza vichochoro ambavyo hutumika kama njia za kutoka sehemu moja kwenda nyengine kuwa vyoo ni jambo la hatari sana na halifai uvumiliwa hata kidogo.

Kutokana na malalamiko yaliotolewa na wanachi hao ni vyema Baraza la Manispaa  la mji wa Unguja likajenga vyoo kwa ajili ya matumizi ya watu wanaolalamikiwa angalau kupunguza uchafu uliotapakaa sehemu hio na  kuondoa hatari na usumbufu.

Kwa vyovyote vile ujenzi wa vyoo kwa wanaume na wanawake katika maeneo hayo utasaidia kuliondoshea kuliweka eneo hilo katika hali ya usafi na kuondoa lawama zinazotolewa kwa Baraza la Manispaa kwa kulifumbia macho tatizo hili.

Sote tunafahamu kwamba kinyesi ni jambo la kukirihisha sana kikiwa cha haja ndogo au kubwa vinaweza kusababisha maradhi mbali mbali kwa binadamu na ndio sababu zikaekwa sehemu maalum kwa ajili ya kwenda kufanyia haja hizo.