UWANJA wa Mao Zedong uliojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni miongoni mwa viwanja bora vya michezo viliopo visiwani hapa, ukishirikisha michezo kadhaa.

Uwanja huo hivi sasa uendelea kutumika na kutoa faraja kwa wanamichezo mbalimbali nchini baada ya kufunguliwa na rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein.
Kukamilika kwa uwanja huo, kuliongeza idadi ya viwanja vya kisasa kufikia vitatu ukiwemo uwanja wa Amaan na Gombani, Pemba.

Tunaendelea kuwapongeza ndugu zetu wa China kwa namna walivyokubali kuujenga tena uwanja huo baada ya kuchakaa na kupoteza haiba yake kama uwanja pekee uliokuwa ukitumika hata kwenye michuano ya Kombe la Goseji kwa wakati huo.

Lakini kwa ujenzi wa sasa, uwanja huo umejumuisha michezo mengine midogo midogo ya ndani na hivyo kutoa fursa zaidi ya kuendeleza michezo nchini.
Bila ya shaka uwanja huo umepunguza tatizo la kuwepo kwa viwanja vya kisasa vya michezo hasa ya ndani liliopo visiwani hapa.

Lakini pamoja na hali hiyo njema, kulijitokeza tatizo kidogo la kuwepo kwa jaa pembeni mwa uwanja huo na hivyo kwa kiasi kikubwa kupoteza haiba yake na matarajio ya wengi kwamba utakuwa kichocheo cha kukuza na kuimarisha michezo.

Zanzibar Leo kama jamii ya wanamichezo tulikuwa miongoni mwa wale ambao tulilalamikia hilo na kueleza wazi kutoridhishwa na mandhari ya hapo kutokana na kuwepo kwa jaa hilo.
Lakini, sasa tunaweza kusema tumefarijika kwa namna mamlaka husika zilivyoliona tatizo na kuamua kulihamisha jaa hilo ambapo kama utatembelea uwanja huo hivi sasa utaona jinsi unavyopendeza kwa rangi na muonekano wake.

Kwa maneno mafupi na yalionyooka, ni kwamba kitendo cha kutupa taka katika uwanja huo kwa kweli kilikuwa hakikubaliki na hakikuleta picha nzuri na kilitoa doa fulani kwa uwanja huo.
Sasa tunaamini kuondolewa kwa jaa hilo mamlaka zilizohusika zimetimiza wajibu wao na kurejesha haiba ya uwanja huo.

Lazima tufikie mahali na kujikubalisha kwamba mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe na sote tuwajibike katika kuliona hili kwa ajili ya maendeleo ya taifa na wananchi wake.

Tuna imani kubwa kwamba, uwanja huu utaendelea kufungua ukurasa mpya wa kuibua vipaji vipya ambavyo vinaweza kuwika tena katika michezo huku viliopo vikihitaji kuendelezwa ili viweze kuonekana.
Hongera mamlaka husika kwa kuliondoa jaa la Uwanja wa Mao Zedong, Zanzibar yenye mafanikio ya michezo inawezekana ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.