NA KHAMISUU ABDALLAH

KAMPUNI ya simu za mkononi Zantel imezindua Eazy Gazeti ili kurahisisha maisha ya wateja wao kupitia simu za mkononi na kufaidika na huduma zinazotolewa na mtandano huo.

Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo katika hoteli ya Park Hayyat Forodhani, Mkuu wa Zantel Zanzibar, Mohammed Khamis Mussa ‘Baucha’ alisema hatua hiyo ni mfululizo wa mikakati ya Zantel katika kuboresha huduma kwa wateja wake.

Aidha alisema hatua hiyo pia itatoa suluhisho la kidijitali litakaloziba pengo la upatikanaji wa habari muhimu kwa kuwasaidia watu kusoma magazeti kutumia simu zao za mkononi popote walipo hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema lengo la kuzindua huduma hiyo ni kuwapa fursa wateja kupitia simu zao kuona wanapata magazeti wanayotaka kila siku na kusoma taarifa mbalimbali zinazotokea nchini Tanzania.

“Wengi tumekuwa wateja wa kusoma magazeti yetu na hata pale panaojitokeza taarifa muhimu basi tunakuwa tunayakosa na kukuta magazeti yote yameshamalizika sasa hii ni moja ya kutatua chagamoto ya wateja kuona wanapata gazeti katika mtandano,” alisema. 

Baucha alisema magazeti pia yanaweza kutumika kupata kumbukumbu za nyuma, hivyo hatua hiyo ni muhimu kwa mtandao huo katika kuimarisha maisha ya watu.

“Zantel tupo kwa ajili ya kutoa huduma siku 365 za mwaka na kuwafikia wanannchi wote ambao wanatumia mtandao huu,” alisema.

Alisema Zantel ipo katika mkakati wa kuona mikopo wa wanafunzi inalipwa kwa kutumia Eazypesa na hata wakulima wa karafuu wanalipwa kwa kutumia huduma hiyo na ZSTC.

Alisema Zantel imejipanga kutoa huduma za kidijital na kuona wateja wote wanakwenda sambamba na mfumo huo, hivyo aliahidi kuwa Zantel itaendelea kurahisisha wateja wake ili kutoa fursa kwa wateja kufanya shughuli nyengine za kimaendeleo.

“Tumeanza na huduma ya kununua umeme, kulipia maji, kununua tiketi za boti na leo tumezindua huduma ya Eazy Gazeti kwa kutumia Ezypesa. Hii yote ni kuona tunarahisiha maisha ya wateja wote na kunufaika na huduma zetu tunazozitoa,” alisema 

Aliwaomba wananchi ambao bado hawajajiunga na mtandao huo kujiunga mapema ili kutumia fursa m zinazotolewa na mtandao wa Zantel.

Nae, Meneja Biashara wa Eazy Gazeti Tanzania kutoka kampuni ya ‘Smart Code’ Johahhes Julias Lutachalwa, alisema wameungana na Zantel ili kuwa na teknolokujia ambayo itawarahisishia wateja wao kupata taarifa mbalimbali kiganjani mwao.