NA KHAMISUU ABDALLAH

JUMLA ya wageni 4,366 wameingia nchini mwezi Agosti, mwaka huu, ukilinganisha na wageni 68,163 kwa mwezi huo mwaka jana ambapo idadi ya uingiaji wa wageni imepungua.

Takwimu hizo zilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Utalii Abdulmalik Bakar Ali wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika ofisi ya Mtawimu mkuu wa Serikali Mazizini.

Aidha alisema asilimia 61.7 ya wageni walioingia nchini mwezi uliopita walitoka bara la Ulaya sawa na ongezeko la asilimia 35.2 ukilinganisha na mwezi wa Julai mwaka huu ambapo jumla ya wageni walioingia nchini walikuwa 3,079.

Akizitaja nchi iliyoongoza kuleta wageni ni Ufaransa ambapo ilichangia asilimia 15.3 ya wageni waliongia nchini ikifuatiwa na Marekani iliyochangia kwa asilimia 9.2.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa mwezi Agosti asilimia 77.0 ya wageni walipita Uwanja wa ndege na asilimia 23.0 walipitia bandarini kati ya hao asilimia 45.4 walikuwa wanaumme na wanawake walikuwa ni asilimia 44.6.

Sambamba na hayo, alisema asilimia 7.8 ya wageni walikuwa chini ya umri wa miaka 15 asilimia 89.6 ni wenye umri wa miaka 15 hadi 64 na asilimia 2.6 ni wenye umri kuanzia miaka 65 na kuendelea.

Nae mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA Dk. Estella Hassan, alisema licha ya nchi kukumbwa na maradhi ya korona, lakini uingiaji wa watalii nchini kwa mwezi huu kiwango chake sio kibaya.

Sambamba na hayo, alisema Idara ya Uhamiaji Zanzibar, imeweka mfumo maalum wa kielekroniki, ili kupunguza msongamano kwa wageni wanaokuja nchini tokea kuanza kwa maradhi ya korona.

Meneja Benki Kuu ya Tanzania BOT tawi la Zanzibar, Moto Nwinganele, alisema serikali imefanya uchunguzi kupitia wizara ya fedha na kubaini changamoto ya kiuchumi zilizotokana na maradhi ya korona.

Alisema katika kutatua changamoto hiyo serikali ilipunguza baadhi ya kodi na nyengine kuzuiliwa kulipa kabisa mpaka hali ya kiuchumi itakapokaa sawa kwa kuwasaidia wawekezaji wanaotegemea sekta ya utalii.