Zanzibar kuadhimisha leo Maulid ya Mtume

NA MWANDISHI WETU

SHUKRAN zote anastahiki kuabudiwa yeye Mwenyezi Mungu bwana wa ulimwengu wote na Mtume Muhammad (SAW) na mjumbe wake.

Huu ni mwezi wa mfungo sita mwezi ambao amezaliwa Mtume wa waislamu wote duniani Muhammad (SAW) ambapo alizaliwa mwezi 12.

Kwa mwaka huu Zanzibar inaadhimisha maulid ya Mtume (SAW) leo hii kutokana na uchaguzi mkuu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kushabihiana kabisa na siku chache za uchaguzi.

Kwa kawaida Serikali ya Mapinduzi Zanzibar huadhimisha mkesha wa kuamkia mwezi 11 mfunguo sita ya kila mwaka kusoma maulidi ya kitaifa ya kuzaliwa kwa mtume na baadae kusomwa maulisi katika madrasa na mitaa mbalimbali kama ilivyo kawaida.

Katika Makala yetu hii leo tutaangazia historia ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kama inavyojulikana na waislamu kuwa mwezi huu wa mfungo sita ndipo alipozaliwa kipenzi cha waislamu wote duniani.

Baba yake Mtume (S.A.W.) amezaliwa mwaka wa 545 A.D. alikua ni mtoto wa kumi 10 katika ndugu 12 wanaume.

Ama ndugu zake wote wanaume na wanawake ni 14. Yeye alikua ni baba mmoja mama mmoja na Bwana Abu Talib, baba yake Sayyidna Ali (Khalifa wa nne), lakini Bwana Abu Talib alikua mkubwa kuliko yeye kwa miaka mitano.

Alipotimia miaka 24 na kitu, baba yake Bwana Abdul Muttalib, alimposea Mwana Amina bint Wahab – alikua miaka 24 –. Wakaingia nyumbani awali ya mwezi wa Rajab, Agost 570, A. D. Mwezi ule ule bibi huyu alishika mimba ya Mtume (s.a.w.).

Hata ulipokua msafara mdogo wa Kikureshi unatoka kwenda Sham kufanya biashara, baba yake Bwana Abdul Muttalib, alimuamrisha atoke pamoja nao akafanye baadhi ya biashara, ili wapate pesa za kufanyia karamu wakati atakapozaliwa huyo mtoto, kwani mtoto huyo atakua ndiye mtoto wake wa kwanza, kifungua mlango wake.

Akenda mpaka Sham na akafanya biashara yake kama alivyoamrishwa na baba yake. Hata wakati wa kurejea, alipofika Madina, alishikwa na homa ya malaria – Madina ilikua mashuhuri kwa homa ya malaria – Akakaa kwa wajomba wa baba yake, Bani Najjar. Kwani tumekwisha kuona kuwa mama yake Bwana Abdul Muttalib ni mwanamke wa Kimadina.

Akaugua kwa muda wa mwezi mzima, kisha akafa katika Mfunguo nne. Akazikwa huko huko Madina katika nyumba ya jamaa yake aliyekua akiugulia kwake siku zote. Alipokufa alikua ni kijana wa miaka 25 na kitu.

Wakati huo alipokufa baba yake, Mtume (s.a.w.) alikua mtoto wa matumboni wa miezi minane – Kama wenye Tarehe[1] wengine wanavyothibitisha, si mtoto wa matumboni wa miezi miwili kama alivyo sema mwenye Maulidi ya Barzanji na wengine.

Mwana Amina alichukuliwa na Bwana Abu Talib, shemeji yake, akakaa eda nyumbani kwake. Baada ya mwezi na kitu akamzaa Mtume (s.a.w.)  nyumbani kwa Bwana Abu Talib, katika mtaa unaoitwa Suqu Al-layl, mtaa wa Bani Hashim.

Alizaliwa alfajiri ya Jumatatu mwezi 12 Mfunguo Sita katika mwaka walioazimia Mahabushia kuuteka mji wa Makka – baada ya kua Yaman yote imo chini ya mikono yao – . Lakini Mwenye-ezi-Mungu aliwaletea ndui, yakaangamia majeshi yao kwa muda mdogo, wakapukutika kama kuku.

Hivi ndivyo alivyosema Askalany katika Al-Bukhary, na ndiyo kauli aliyoitilia nguvu Sheikh Muhammad Abdoo katika tafsiri yake –. Na siku hii ya kuzaliwa kwake inawafiki mwezi 20 April 571.

Kama alivyo hakikisha haya mwanachuoni mkubwa wa Misr – Mahmoud Basha Al-Falaky –. Na siku hii ya kuzaliwa kwake palitokea ajabu kubwa, kama tunazozisikia vitabuni, kwani yeye ni Mtume, na kila Mtume ana miujiza yake.

Wala si uhodari kwa mtu kukanusha kila asilolijua na lisiloingia katika akili yake. Bali uhodari ni kujitahidi kufahamu. Ikiwa mtu hakuiona “Television” wala haiwezi kuingia katika akili yake ndio atasema ni “Uongo, hapana kitu cha namna hiyo!” Basi na akatae vingi visivyoweza kuingia katika akili yake fupi.

Pale pale alfajiri alipokwisha kuzaliwa Mtume (s.a.w.), alikwenda kuitwa babu yake kuja kumuona mjukuu wake, Babu huyu alifurahi sana, na akamfunikafunika maguo mjukuu wake, akajikongoja naye mpaka kwenye Al-Kaaba.

Akafungua mlango, akaingia naye ndani akasimama anamuombea dua kwa mashairi mazuri ya kiarabu aliyotunga mwenyewe wakati ule ule. kisha akarejea naye, na jua bado halijachomoza.

Hata siku ya saba au ya nane alifanya karamu kubwa, na akampa mjukuu wake jina la Muhammad, yaani mwenye kushukuriwa kwa vitendo vyake vizuri. Jamaa zake walipomuuliza sababu ya kumwita jina hili, aliwajibu ya kuwa anamtarajia afikilie cheo hicho cha kushukuriwa na kila mtu. Jina hili kabisa halikua likitumika katika nchi ya Bara Arabu.

Hata ilipokua karibu atadhihiri Mtume (S.A.W.). Mapadiri wa Kinasara na Makohani wa Kiyahudi waliokua wakikaa Bara Arabu walikua wakiwatahayarisha majirani zao wa kiarabu waliokua wakiabudu masanamu, Wakiwaambia: “Karibu ataletwa Mtume katika nchi hii yenu, abatilishe hii ibada yenu mbovu ya masanamu” Walipoambiwa hivi wale waarabu waliwauliza nini litakua jina la Mtume huyo, wakawajibu kuwa jina lake litakua Muhammad. Kwa hivyo kila mwenye kusadiki hayo alimwita mwanawe Muhammad.

Lakini hayakusikilizwa majina haya ila kwa baadhi ya waarabu waliokua wakikaa Sham tu na Najran (Yaman) ambako  Mapadri wengi wa kinasara wakikaa, na vilevile katika Madina ambayo ilikua nusu ya wakaazi wake ni Mayahudi.

Hata lilipoanza kutangaa jina la Mtume wetu (S.A.W.), waliokuwa wamekwisha kuitwa kwa jina hili ni watu kidogo tu Bara Arabu nzima.

KULELWA KWA MTUME (S.A.W).

Mtume Muhammad (s.a.w) alizaliwa katika mji mtakatifu unaoitwa Makka mwaka wa 570 AD.Mwaka huu ulijulikana kama mwaka wa Tembo.Mtume Muhammad (s.a.w) alizaliwa katika Familia  ya Kiarabu yenye heshima kubwa sana na iliyokuwa maarufu sana kila sehemu.

Baba yake Mtume (S.A.W) ni Abdullah,baba yake huyu alifariki dunia kabla ya kuzaliwa kwake.

Pia Mtume (S.A.W) alimpoteza Mama yake mzazi alipofikisha umri wa miaka sita Baada ya miaka miwili au alipofikisha umri wa miaka minane, Babu yake {Abdul Mutw-twalib},aliyempenda sana Mtume na aliyekuwa msimamizi wake naye pia aliaga dunia.

Baadaye Mtukufu Mtume (S.A.W) aliwekwa chini ya usimamizi na ulinzi wa baba yake mdogo Abu Twalib {ambaye ni Baba yake Amirul-Muuminina Ali -a.s-}.

Na huu ulikuwa ni usia wa Babu yake Mtume (S.A.W) kwa mwanae huyo Abu Twalib ambapo alimtaka asimamie maisha yake (S.A.W) na kumpa ulinzi wa kutosha dhidi ya maadui wabaya waliokuwa na lengo la kutaka kumdhuru Mtume (S.A.W),usia huu baada ya kifo cha {Abdul Mutw-twalib},{Abu Twalib} aliufanyia kazi ipasavyo.

Abu Twalib alimpenda sana Mtume (S.A.W) kama vile alivyowapenda watoto wake bila ya kumbagua na wakati mwingine alizidisha mapenzi kwa Mtume (s.a.w) kuliko hata watoto maana likuwa halali mpaka anahakikisha Mtume (S.A.W) ubavuni mwake na mengine mengi ambayo yalionyesha ni jinsi gani anavyotilia umuhimu maisha ya Mtukufu Mtume (S.A.W).

Hadi miezi michache kabla ya Hijra (yaani kabla ya kutoka Makka kwenda Madina), Abu Twalib (Mwenyeezi Mungu amrehemu) alikuwa akifanya kila awezalo kwa lengo la kuhakikisha anamhami Mtume Muhammad (S.A.W) na hakupumzika hata kidogo.

Kama walivyokuwa waarabu wengineo,waarabu wa Makka walijishughulisha na ufugaji mbuzi, kondoo na ngamia.Walikuwa pia wakifanya biashara na nchi jirani na Makka kama vile Syria.Walikuwa watu wasiojua kusoma wala kuandika na hawakufanya juhudu zozote zile za kuwaelimisha watoto wao.

Kama vile watu wake wote, Mtume Muhammad (S.A.W) pia hakuwa amejifunza kusoma wala kuandika,lakini tangu mwanzoni mwa maisha yake alifanikiwa kuwa na sifa nzuri sana na nyingi sana.

Hakuwahi kuabudu masanamu,hakuwahi kusema uongo,hakuwa kuiba wala kupora mali za watu wala kufanya khiana.

Alijizuia na uovu,utovu wa nidhamu,pamoja na utovu wa adabu na vitendo vyote vya kuaibisha.Alikuwa mwerevu na mwenye bidii.

Kwahiyo alipata umashuhuri sana na kupendwa sana na watu katika kipindi cha muda mfupi sana ambapo watu {kwa  harakaharaka} kutokana na tabia nzuri zisizokuwa na kifani walizoziona kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na ambazo walikuwa hawajawahi kuziona kwa binadamu yeyote kabla yake ziliwafanya wakaamua kumbandika jina la “MUHAMMAD MWAMINIFU”.Kwa kawaida Waarabu walikuwa wakimwachia amana zao na kuzungumzia kila mara juu ya uaminifu wake na bidii yake.

Mtume Muhammad (S.A.W) alipokuwa na umri wa miaka karibia ishirini (20) Mwanamke mmoja,Tajiri mkubwa wa Makka,aliyekuwa akiitwa Khadija Al-kubra, baada ya kuona sifa nzuri za Mtume (S.A.W) na uaminifu wake wa hali ya juu, alimchangua Mtume Muhammad (S.A.W) kuwa mwakilishi wake katika masuala ya biashara zake.

Mwanamke huyu alipata faida kubwa sana kutokana na ukweli,uaminifu na busara na bidii ya Mtume Muhammad (S.A.W).Bila shaka Mwanamke huyu aliendelewa kuvutiwa zaidi na shakhsia na adhama ya Mtume Muhammad (S.A.W) na hatimaye kutoa pendekezo la kutaka kuolewa na Mtume Muhammad (S.A.W).Mtume Muhammad (S.A.W) alikubali pendekezo hilo,na katika umri wa miaka  ishirini na tano (25) akamuoa Mwanamke huyo aliyekuwa tajiri mkubwa.

Miaka mingi baadaye,pia aliendelea kufanya biashara na Mtume Muhammad (S.A.W) ambaye sasa ni mumewe tiyari.

Akiwa akichukuliwa kuwa ni mmoja kati ya watu,Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu (S.W) Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na uhusiano wa kawaida na watu ahadi alipofikisha umri wa miaka arobaini (40).

Bila shaka alikuwa akitofautiana na watu hao katika nukta kadhaa ambapo tunamkuta Mtume (S.A.W) alikuwa na sifa nzuri na aliepuka vitendo viovu na pia uhusiano mbaya uliowapoteza wengi.

Mtume (S.A.W) Hakuwa mtu wa shari,hakuwa na moyo mgumu,hakujidai,hakuringa na wala hakujiona mbora kuliko wengine kitu ambacho kiliwafanya watu kumpa heshima kubwa na kumwamini.

Siku moja Waarabu walipokuwa wakijenga upya Kaaba Tukufu,kulitokea ugomvi mzito wa kutosikilizana kati ya makabila kuhusiana na uwekaji wa jiwe Jeusi mahala pake katika Kaaba hiyo Tukufu.Kila kabila linataka ndilo liwe lenye kuweka jiwe hilo katika mahala pake kwenye Kaaba hiyo Tukufu.

Hivyo ikawa ni nivute nikuvute na amani ikawa iko hatarini kutoweka kati yao.Watu waote wakamchagua Mtume (S.A.W) kuwa msuluhishi wa ugomvi huo.

Mtume (S.A.W) aliwaamuru watu hao (waliokuwa wakivutana katika ugomvi huo ambao kidogo tu wapigane kama sio Mtume (S.A.W) kuwasuluhisha) waliweke jiwe hilo Jeusi {ALHAJARUL-AS-WAD} katika shuka lenye ncha nne,kisha akawaamuru wakuu wa makabila hayo kila mtu ashike pembe ya shuka hilo na kunyanyua shuka hilo juu.

Wakuu wa makabila hayo wakafanya hivyo na kulinyanyua shuka hilo lililokuwa na jiwe hilo Jeusi kisha Mtume (S.A.W) akapanda juu ya kaaba mpaka usawa wa kukaa jiwe hilo na kulipokea jiwe hilo Jeusi na kuliweka mahala pake kwenye Kaaba hiyo Tukufu ambako mpaka leo hii jiwe hilo liko mahala pale.

Kwa njia hii Mtume (S.A.W) akawa ameumaliza ugomvi na kukata mzizi wa fitina bila ya kutokea mauaji yoyote ya umati wala kumwaga damu.

Hata kama Mtukufu Mtume (S.A.W) alikuwa akimwabudu Mwenyezi Mungu (S.W) na kujiepusha kuiabudu miungu kabla ya kubaathiwa au kabla ya kutumwa kuwa Mtume, watu hawakumjali kwa vile hakutangaza wazi wazi mapambano yake dhidi ya imani na itikadi (za kijaahiliyya) zisizokuwa na msingi.

Hali hiyo pia ilihusika na wale waliokuwa wafuasi wa dini nyinginezo kama vile wayahudi, na wakristo ambao waliishi kwa heshima miongoni mwa Waarabu bila ya kusumbuliwa na Waarabu.