WASHINGTON, MAREKANI

MKURUGENZI wa Idara ya ujasusi Marekani John Ratcliffe amesema  kwamba Urusi na Iran zimejaribu kuingilia kati uchaguzi ujao wa rais unaotarajiwa kufanyika rasmi Novemba 3.

Katika mkutano na waandishi habari, Ratcliffe alisema Iran na Urusi zimeweza kupata baadhi ya taarifa za usajili wa wapiga kura.

Aidha aliongeza kwamba maofisa wa Serikali tayari wamegunduwa kwamba Iran ilituma barua pepe zinazolenga kuwatisha wapiga kura, kuchochea machafuko katika jamii na kuchafuwa jina la Rais Donald Trump.

Ofisa mmoja wa ujasusi alisema barua pepe hizo bado zinafanyiwa uchunguzi, na hakuna uhakika ni nani aliyezituma.

Awali, mashirika ya ujasusi ya Marekani yalionya kuwa Iran inaweza kuingilia kati uchaguzi ujao ili kumuumiza Trump na kwamba Urusi itajaribu kumsaidia Trump katika uchaguzi huo.