JERUSALEMU,ISRAEL

ISRAEL na Umoja wa Falme za Kiarabu, zimekubaliana juu ya utaratibu wa kusafiri baina yao bila kuhitaji viza, wa kwanza kati ya Israel na taifa la Kiarabu.

Makubaliano hayo yalisainiwa baada ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu kuafikiana kurekebisha uhusiano wao katika makubaliano yaliyosainiwa ikulu ya Marekani mwezi uliopita.

Wakati ambapo chumi zao ziliathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona, Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu zinatarajia manufaa ya haraka kutokana na makubaliano ya kurekebisha uhusiano baina yao ambayo yalivunja muafaka wa miaka kadhaa wa mataifa ya Kiarabu kwamba hakupaswi kuwa na uhusiano na taifa hilo la Kiyahudi hadi lifikie amani na Wapalestina.

Umoja wa Falme za Kiarabu ilikuwa nchi ya tatu ya Kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel, na kufuatiwa muda mfupi na Bahrain. Nchi nyengine zenye uhusiano na Israel ni Misri na Jordan.