NA MWAJUMA JUMA

MWENYEKITI wa Bodi ya Kituo cha Msaada wa Kisheria na Kijamii kwa Wazee Zanzibar, Jaji Mshibe Ali Bakari, amesema uchaguzi uliofanyika una umuhimu mkubwa, kwani ni njia mojawapo ya kutengeneza viongozi watakaoijenga nchi.

Jaji Mshibe ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, aliyasema hayo katika kongamano la kujadili nafasi ya wazee katika uchaguzi mkuu lililofanyika katika skuli Shaa, mjini Unguja.

Alisema kuna watu wanalichukulia mzaha suala hilo, lakini waelewe kwamba uchaguzi ni mabadiliko ya uongozi ambao unakua katika hali ngumu.

“Nchi kufanya uchaguzi maana yake ni tunatayarisha uongozi mwengine,hilo ndio jambo muhimu katika nchi,”alisema.

Alisema watu wanapaswa kutambua kwamba nchi inajengwa na mwananchi mwenyewe na sio mtu mwengine kuja kuwajengea na ikitokea hivyo kukaribisha kutawaliwa.

Aidha aliwataka wazee hao kutambua kwamba wanapokwenda kupiga kura wajuwe kuwa wanachagulia watoto wao ambao hawajatimia umri wa kupiga kura.

Kwa upande wa viongozi wa dini Sheikh Fadhil Soraga na Bishop Michael Hafidh wakitoa ujumbe kwa uchaguzi huo waliwataka wazee hao kuwahamasisha watoto kushiriki katika uchaguzi kwa amani.