HABIBA ZARALI, PEMBA

WANANCHI Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba, wameshauriwa kuzidisha usafi katika maeneo yao yanayowazunguka, ili kuweza kuepuka kujitokeza maradhi ya mripuko yakiwemo matumbo ya kuharisha.

Ushauri huo, umetolewa kwa nyakati tofauti na wananchi Wilayani humo, walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari mara baada ya kujitokeza mvua katika maeneo mbalimbali Wilayani humo.

Wananchi hao walisema ni vyema kila mmoja kuchukuwa tahadhari za kudumisha usafi kwa makusudi, ili kuepukana na maradhi hayo hatari ambayo kuwepo kwake yanaweza kupoteza maisha ya watu.

Juma Saidi Mkaazi wa Makombeni, alisema maradhi ya kuharisha yanapoingia hayachagui mkubwa wala mdogo, hivyo ni vyema kuwa makini katika harakati za maisha yao kwa kuzingatia usafi.

Alieleza kwa wananchi wenye akili timamu si vizuri kusubiria kujitokeza tatizo na kuanza kulaumu viongozi ama Serikali, na badala yake ni vyema kuchukuwa tahadhari mapema, ili kuepusha tatizo hilo kujitokeza.

Akigusia kuhusu wafanyabiashara wa vyakula, Fatma Bakar Mohamed mkaazi wa Mkoani alisema, ni vyema wakachukuwa tahadhari ya kufunika vizuri, ili kuepusha wadudu wanaoweza kueneza maradhi hayo.