NA LAILA KEIS

TIMU ya Jang’ombe Boys kwa mara ya kwanza imefanya uchaguzi wa kidemokrasia uliwachagua viongozi mbali mbali wa klabu hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Rais wa timu Ali Othman Ali alieleza kuwa hatua hiyo itachangia kasi ya mabadiliko na maendeleo ya timu hiyo

Aliwashukuru wanachama wa klabu hiyo kwa kujitokeza kwa wingi na kufanya uamuzi wa kuchaguza viongozi watakaokuwa na jumumu la kuiongoza klabu hiyo yenye mashabiki wengi visiwani hapa.

“Uchaguzi ulioshirikisha wanachama 108, ambao walinichagua mimi kuwa rais wa klabu kwa kura 99 huku ndugu yangu Ali Mohammed Ali akishika nafasi ya Makamu wa Rais, ambae alipata kura zote 108,” alisema Othman.

Mbali ya viongozi hao, alieleza kuwa katika uchaguzi huo, wanachama pia walichagua katibu mkuu na wajumbe wa kamati tendaji wa klabu na kuaahidi kuwa watashirikiana na kuongoza kwa juhudi na maarifa ili kuirudisha ligi kuu na kuchukua ubingwa.

Akizungumzia mchakato huo, Makamu wa Rais wa timu hiyo, Ali Mohammed alisema watahakikisha wanaweka mazingira mazuri yatakayowaunganisha viongozi na wanachama wa timu hiyo ili kuondosha migogoro na kuiletea heshima timu yao.

“Tutaweka mazingira rafiki ya kuongoza timu ili ifikie lengo tulilojiwekea ambalo ni kufanya uchaguzi wa kidemokrasia badala ya kuteuana tu,” alisema.