PARIS,UFARANSA

JAPANI na Ufaransa zimekubaliana kufanya kazi pamoja katika nyanja mbalimbali, ikiwa pamoja na masuala ya Bahari za China Mashariki na Kusini,ambapo China inaongeza shughuli za baharini.

Waziri wa Mambo ya nje wa Japani Motegi Toshimitsu na mwenzake wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian walifanya mazungumzo kwa takribani saa tatu wakati wa chakula cha usiku nchini Ufaransa.

Motegi alitoa wito wa uhusiano imara kwenye masuala mbalimbali, ikiwemo ufikiaji wa eneo huru na la wazi la Indo-Pasifiki kulingana na utawala wa sheria.

Le Drian alisema kwamba anataka kukuza ushirikiano wa nchi hizo mbili katika eneo la Indo-Pasifiki.

Mawaziri hao walikubaliana kwamba nchi hizo mbili zitafanya kazi pamoja katika kukabiliana na virusi vya corona na zitajiandaa kwa dunia ya baada ya janga hilo.

Walikubaliana kwamba mataifa yao yatakuwa na jukumu muhimu kama kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani katika kurejesha uchumi wa dunia na kutengeneza utaratibu mpya wa kimataifa duniani baada ya virusi vya corona.