KIGALI, RWANDA

MKE wa rais wa Rwanda, Jeannette Kagame amezindua kampeni ya kitaifa nchini humo itakayohakikisha nchi inapambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Jeannette alizindua kampeni hiyo ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto kike iliyoadhimishwa hapo juzi.

“Hatuwezi kusherekea vyema siku ya kimataifa ya mtoto wa kike, huku tukijifanya kuzisahau changamoto zinaowakabili watoto wa kike likiwemo jenga la udhalilishaji wa kijinsia wanaofanyiwa”, alisema Jeannette.

Alisema Rwanda inakabiliwa na janga la vitendo vya udhalilishaji wa watoto na kwamba ili kufanikiwa katika kampeni hiyo mpya kila mwananchi wa taifa hilo lazima ashiriki katika kukabiliana na janga la udhalilishaji.

“Hii si kampeni mpya kuzinduliwa nchini kwetu, kampeni kama hizi zimeshazinduliwa nyingi, lakini hatutachoka katika tukiamini tunaweza kulimaliza tatizo hili”, alisema.

Alisema watoto wengi wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wamekuwa wazito kuripoti vitendo hivyo kutokana na kuhofia unyanyapaa.

Ripoti kutoka nchini humo zinaeleza kuwa asilimia 25.5 ya wasichana wameripotiwa kupata ujauzito.