NAIROBI, KENYA

MAMLAKA jijini Nairobi, zimesema kuwa mtu yoyote atakayepatikana akitema mate ama kupenga kamasi bila kutumia kitambaa jijini Nairobi, atahukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani au kutozwa faini ya shilingi 10,000, fedha za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mswada uliowasilishwa na diwani wa wadi ya Rirura, James Kariba katika bunge la kaunti ya Nairobi, unaeleza kuwa adhabu kama hiyo atapewa mtu yoyote atakaye patikana na hatia dhidi ya vitendo vya ukahaba.

Mswada huo, ambao uko katika awamu ya kwanza, unalenga kuchukua mahali pa sheria za jiji la Nairobi, ambazo zimepitwa na wakati baada ya mfumo wa ugatuzi kuanza kutekelezwa.

Katika mswaada huo, Kiriba alisema wale watakapatikana wakiendesha gari au pikipiki kwenye njia zilizotengwa kwa watumiaji miguu pia wataadhibiwa.

Aidha kufanya haja kubwa ama ndogo kwenye barabara za jiji ama maeneo ya umma, kuwasha moto kwenye barabara za umma ama za jiji bila ruhusa ya katibu wa kaunti pia kutachukuliwa kuwa hatia.

Makosa mengine yaliyoorodheshwa katika mswaada huo ni kuacha mbwa ovyo kwenye barabara, kuosha ama kurekebisha gari kwenye barabara za jiji, kuvuta sigara kwenye maeneo ya umma na makonda kuwapigia kelele abiria.

Kuchuuza, kuuza, kusambaza ama kutangaza maandishi yoyoye ama hafla katika barabara ya umma, kupiga kelele ama kutumia kengele, spika ama chombo chochote kile cha kupaaza sauti ama kuendesha gari ili kutangaza bidhaa bila kibali pia kumeorodheshwa kama kosa.

Kwa mujibu wa mswaada huo, atakayefanya kosa miongoni mwa yaliyoorodheshwa hapo juu atakuwa kwenye hatari ya kuhukumiwa miezi sita gerezani, kupigwa faini ya Sh10,000 ama kupewa adhabu zote mbili.