NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ametoa agizo kwa waziri wa TAMISEMI na watendaji wake wausimamie mradi wa kituo cha kisasa cha mabasi kinachojengwa Mbezi Luis, ukamilike mwezi ujao.

Kauli hiyo aliitoa jana, jijini hapa, katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha mabasi – Mbezi Luis, akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Malawi, Dk. Lazarus McCarthy Chakwera, ambae alikuwa ziarani nchini Tanzania.

Alisema mradi huo lazima umalizike mwezi ujao na visiwepo visingizio vya mripuko wa ugonjwa wa coroma, mvua, jua au matope hivyo wajenge usiku na mchana mradi umalizike.

Aidha Dk. Magufuli alimuagiza mkurugenzi wa jiji, ambae aliyeweka saini mkataba huo na mkandarasi wasimamie ukamilishwaji wa ujenzi huo hasa ikizingatiwa kila kinachohitajika kipo.

“Mkataba huo ni wa shilingi bilioni 71, ulikuwa umalizike mwezi Julai), lakini hadi sasa tupo mwezi Oktoba mradi haujesha kisingizio ugonjwa wa corona, wanasema utamalizika mwezi Januari miezi minne kutoka sasa nani atafidia fedha kipindi hicho?” alihoji.

Alieleza kuwa mkandarasi anapaswa akatwe pesa kwa kuchelewesha mradi huo na kuwakumbusha viongozi wa Dar es Salaam wasimamie miradi ili imalize kwa wakati.

Alifahamisha kuwa mradi huo utakapofanya kazi kutakuwa na maegesho ya mabasi 1,000, TAXI 280 kwa siku, kutakuwepo maeneo ya bodaboda, bajaj na eneo la mama lishe ambapo walitakiwa wawe wameshaanza kazi tangu mwezi wa Julai.

Magufuli alisema anaelewa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ni mgeni hata hivyo, anatakiwa abadilike awe mkali, asiwe mpole asimamie watu watimize wajibu wao.

Hata hivyo aliwaeleza ataufuatilia mradi huo ili kujua kama kuna ubadhirifu kutokana na kutumia shilingi bilioni 71 wakati pesa alizoidhinisha baada ya baadhi ya watendaji na madiwani walikuwa wanagombana kwa mradi huo ni shilingi bilioni 51.