RAIS John Pombe Magufuli amewafuta machozi walimu, wastaafu na baadhi ya wananchi kwa kuokoa na hatimaye kuwakabidhi mali na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 82 walizokuwa wametapeliwa kupitia Kampuni za Mikopo zinazoendesha shughuli zake kinyume na utaratibu.

Mkuu wa Mkoa Dk Rehema Nchimbi, kwa niaba ya Rais, amewakabidhi
kiasi hicho cha fedha waathirika wote waliopitiwa na wimbi hilo, maarufu ‘Mikopo Umiza,’ ofisini kwake.

“Ni Serikali hii ya Magufuli ndio iliyofanikisha kuwabana hawa wakopeshaji haramu na hatimaye leo walimu wangu na ninyi watumishi wenzangu mnakabidhiwa haki yenu iliyokuwa imeporwa, tuendelee
kumshukuru Rais kwa mema haya anayoendelea kutufanyia,” alisema Nchimbi na kuongeza:

“Rais Magufuli mda mrefu alishakampeniwa na Mwenyezi
Mungu mwenyewe kupitia Corona, kama Mungu alipitishia kwake ile neema, maono na uwezo ule wa kusimama bila kutetereka, mimi Rehema Nchimbi ni nani hata nisiendelee kumsifu?” alihoji.Akiwasilisha taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema takribani shilingi milioni 82.8 pamoja na mali nyingine vimeokolewa na kurejeshwa kwa wahusika. 

Alisema matokeo ya ufuatiliaji na udhibiti huo umebaini kuwa baadhi ya wakopeshaji binafsi wanafanya shughuli hiyo bila ya vibali halali, hali inayosababisha kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato na kujipatia fedha isivyo halali.

Pamoja na mambo mengine, alisema udhibiti umebaini kuwepo kwa utozaji mkubwa wa riba zisizovumilika za zaidi ya asilimia 100 kinyume na viwango vilivyowekwa na kuainishwa na Benki Kuu, sanjari na wakopeshaji kukaa na kadi za benki za wakopeshwaji kwa lengo la kuchukua fedha kila ifikapo mwisho wa mwezi.