NA MWANAJUMA ABDI

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli amesema kugombea katika vyama tofauti sio uadui, na kwamba wenye dhana hizo waziondoshe kwenye mawazo yao.

Kauli hiyo aliitoa jana, wakati akizungumza na wanaCCM na watanzania huko Mwanga mkoa wa Kilimanjaro, katika muendelezo wa mikutano ya kampeni zinazoingia kwenye ngwe ya lala salama.

Mgombea huyo aliwaeleza wanaCCM na wananchi wa Mwanga, kuwa wagombea wanaohubiri uadui hawafai kuchaguliwa kuwa viongozi.

Aliwataka wananchi wa Mwanga na mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha wanakichagua Chama cha Mapinduzi kwani kina azma ya kuwaletea maendeleo wananchi sambamba na kusimamia amani.

Alisema Jumatano ijayo wajitokeze kwa wingi wote waliojiandikisha kwenda kupiga kura, waangalie vizuri katika karatasi ya kupigia kura na wakifika waweke alama ya vyema katika eneo la chama cha mapinduzi.

“Ukienda sehemu ya pili utakuta jina la mgombea na Makamu wa Rais utamkuta mama mmoja mzuri mweupe, Mama Samia Suluhu Hassan na ukienda sehemu inayofuata utamkuta mgombea Urais Dk. John Pombe Magufuli na mwishoni utaweka alama ya vyema na ukishamaliza usihangaike kuangalia picha nyengine”, alisema.

Alisema amefarajika na wananchi wa Mwanga kwa vile hawajawahi kumuangusha kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano wake wa kampeni kwa ajili ya kuwaombea kura wanaCCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani kwa chama cha Mapinduzi.

Alitoa wito kwa watanzania wanapomaliza kupiga kura siku hiyo, ambayo itakuwa ni ya mapumziko warudi majumbani kwa ajili ya kuzingatia amani.

Alisema amani ni kitu kikubwa sana, ambapo alisisitiza asije kutokea mtu baada ya kupiga kura akakwaambia nenda kafanye fujo au kafanye maandamano, kachome majengo, kaweke matairi barabarani mtu huyo atakuwa anakuweka katika eneo baya.

Akigusia miradi ya maendeleo katika wilaya ya Mwanga, alisema atahakikisha mradi mkubwa wa maji unaogharimu shilingi bilioni 262 unamalizika kutoka nyumba ya mungu hadi Mwanga na Same ili kuwapatia maji safi na salama wakaazi wa hapo na maeneo jirani.

Alisema atamsimamia mkandarasi mwenyewe, ambaye alipewa kazi hiyo tokea mwaka 2014 -2015 na ulitakiwa kumaliza mwaka 2017 lakini mpaka sasa ametekeleza kwa asilimia 64, hivyo wakimpa miaka mitano tena ya urais atalishughulikia hilo.

Alieleza tayari ameshatoa maagizo kwa Naibu Waziri wa Maji na watendaji wa maji kuufuatilia mradi huo na halafu wampelekee mrejesho wa mkandarasi huyo alivyopanga kukamilisha.