NA ZAINAB ATUPAE

 KAMATI ya Rufaa na Usuluhisho imetupilia mbali rufaa ya Uhamiaji na kukubaliana na maamuzi yaliotolewa na kamati ya kusikiliza malalamiko ya awali.

Rufaa hiyo alikatiwa mchezaji Nassir Ali Hemed ambaye alikuwa na uhalali wa timu ya Danger na kuhamia katika klabu ya Black Sailor kwa kufuata taratibu zote za usajili.

Kwa mujibu ya barua iliyotolewa na kamati hiyo na kutiwa saini na Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya Awali ZFF Zanzibar Ali Abdalla Ali na Katibu Ahmada Jumbe Marika,walisema baada ya kupokea lalamiko hilo walifanya uchunguzi kwa kina na kugundua mambo matatu.

Kamati ilibaini kuwa mchezaji Nassir Ali Hemed alikua na uhalali kutoka timu ya Danger na kwenda Black Sailor, ambapo risiti  pamoja na fomu zake za uhamisho  kamati iliridhika kuwa ni mchezaji halali wa Black Sailor na si mchezaji wa Aman Academy kama ilivyodai timu ya Uhamiaji.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mchezaji huyo alikuwa huru baada ya Amaan Academy kutoshiriki ligi na kuchukuliwa na Danger na baadaye kujiunga na Black Sailor.

Jambo jingine lililobainika ni kwamba kocha mmoja ya viongozi wa benchi la ufundi la timu ya Uhamiaji FC,alishiriki katika kadhia hiyo ya kuibua hoja  na kupelekea kuwepo rufaa hiyo.

Kamati iligundua kwamba kiongozi huyo alitengeneza kadhia hii kwa kujaribu kuficha ukweli pamoja na kuitengenezea mazingira mazuri klabu yake,ili Black Sailor ionekane ilikiuka taratibu za uhamisho kupitia mchezaji huyo.

Hivyo kamati ya rufaa inakubaliana na maamuzi ya kamati ya kusikiliza malalamiko ya awali kwamba yalikuwa ni sahihi.

Aidha waliwataka wowote ambao hawakuridhika na maamuzi hayo wanayo haki ya kwenda kukata rufaa.