NA KHAMISUU ABDALLAH

TUME ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), imeviasa vyama vya siasa na wagombea kuzingatia maadili ya uchaguzi katika kampeni zao, ikiwemo kuepuka lugha za kashfa na maneno ya uchochezi yanayotishia amani ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na kamishna wa NEC, Asina Omar, katika mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa kituo cha habari na uangalizi wa uchaguzi kilichopo katika Chuo cha Utalii Maruhubi.

Alisema ni jambo la msingi kwa vyama vya siasa na wagombea, kuepuka kufanya kampeni ambazo zina ashiria ubaguzi katika misingi ya jinsia, ulemavu, ukabila, udini, maumbile, rangi na kadhalika.

Kamishna huyo alisisitiza kuwa lengo la vyama vya siasa kuekewa kanuni na maandili ni katika kuhakikisha kila chama kinashiriki kwenye kampeni kwa salama na kupata fursa ya wanachama kushiriki katika mikutano.  

Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi alisema Tume imeweka mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu na makundi mengine yanayohitaji usaidizi kupiga kura bila ya usumbufu.

Akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa wadau wa uchaguzi mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC), Kosmas Mwaisogwa alisema daftari la kudumu lina jumla ya wapiga kura 29,188,347 ambapo wapiga kura 29,059,507 wapo Tanzania bara na 128,840 wapo Zanzibar.

Aidha alisema ZEC imeandikisha wapiga kura 566,352 ambao watashiriki kupiga kura ya kumchagua Rais na Wabunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkurugenzi Kosmas alibainisha kwamba kati ya wapiga kura 29,188,347 walioandikishwa wanawake ni 14,691,743 na wanaumme 14,496,604 ambapo kwa upande wa vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 35, alisema ni 15,650,998 wakiwemo wanaumme 7,804,845 na wanawake 7,846,153.

Hata hivyo, alisema kwa watu wenye ulemavu jumla yao ni 13,211 kati yao 2,223 wana ulemavu wa macho, 4,911 wenye ulemavu wa mikono na 6,077 wana ulemavu wa aina nyengine.