Ili kumea kwa lugha ya Kiswahili nchini, wanasiasa msitumie lugha ya kashfa kwenye kampeni

Na Ali Othman

UCHAGUZI mkuu wa Oktoba 2020 ni miongoni mwa nguzo muhimu katika ujezi imara wa kudumisha demokrasia nchini.

Mjenzi au mkandarasi huyo imara hutegemeana sana na fundi mkuu ambapo kampuni ni Lugha fasaha ya Kiswahili na mkandarasi hapa ni chama au vyama vya siasa, ambavyo kwa sasa vipo mitaani kwa ajili ya kusaka ridhaa ya kuongoza wananchi ambao ndio vibarua wao.

Kwa kuwa kila Mkandarasi amepewa usajili halali wa ujezi wa taifa hili, ni vyema kufahamu kutumia lugha nzuri kwa lengo la kuwavutia wateja yaani wapiga kura badala ya kuwabugudhi na kuwadhalilisha.

Ifahamike kwamba kiswahili ni miongoni mwa lugha muhimu na adhimu katika bara la Afrika na duniani kwa ujumla, ambapo Kiswahili kimeyaunganisha makabila 120 yanayopatikana ndani ya Jamuhiri ya Muungano wa Tanzania.

Licha ya kutokuwepo na orodha kamili ya makabila visiwani hapa, lakini bado Kiswahili kinachukuwa nafasi kubwa ya kuwaunganisha wananchi wa visiwani, ustarabu wa lugha ya Kiswahili ni heshima tosha kwa taifa na hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Uchaguzi ni siku chache lakini heshima na ustarabu ni vitu vya kudumu, hivyo ni maajabu kuona viongozi wa vyama kama kampeni zao kutumia muda mwingi kutukana na kuwakebehi viongozi wenzao hata kama ni wa vyama vingine bado watakuwa ni viongozi hadi mwisho wa uhai wao.

Kalamu za waandishi wa habari na vyombo vya habari, ambavyo kwa asilimia kubwa vimekuwa vikitumia lugha asili ya Kiswahili, vimeweza kuimarisha umoja uliopo sasa tangu mwaka 1961 kupatikana uhuru wa Tanzania.

Kwa upande wa Zanzibar Kiswahili kimegawika katika lahaja tatu muhimu, mbazo ni Kitumbatu, Kimakunduchi na Kipemba. Uwepo wa lahaja hizo, haimanishi kwamba Kiswahili ndio kimepotea au kupotoka la khasha, bali ni ukuwaji na uimara wa lugha ya Kiswahili.

Na ndio maana  Baraza la habari Tanzania mwaka 2016 liliandaa kanuni za maadili kwa wanataaluma wa habari kwa lengo la kuwatanabahisha wamiliki na waandishi wa habari umuhimu wao pamoja na kufuata maadili.

Ili kuona kwamba Kiswahili kinaendelea kuenziwa kumewekwa machapisho kadhaa ambayo ni pamoja na Machapisho yasipotoshe kwa makusudi au kuwaarifu isivyo wasomaji, watazamaji au wasikilizaji kwa kuweka au kuacha kitu kilichokusudiwa. Hakikisha hakuna vitu visivyo na msingi, vinavyopotosha au kukosa ukweli.

Na kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi katika ngazi mbali mbali mbali, kama vile Udiwani, Uwakilishi, Ubunge pamoja na Urais ipo haja ya kusisitizana na kukumbushana kuhusu  matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili.

Kwa mfano unapowasikiliza viongozi wawili wa vyama vikuu vya upinzani hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni wazi kuwa lugha zao hazioneshi kuwa na nia njema hata kidogo, mbaya zaidi vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele kueneza uchochezi na sasa unapoangalia televisheni za mitandaoni ambazo zipo kwenye You tube, sijuwi lengo nini?

Licha ya sheria na kanuni zilizopo kwenye taaluma ya habari, lakini kuna baadhi ya vyombo vya habari kwa makusudi vimekuwa vikienda kinyume na utaratibu huo, ingawaje mara nyingi lawama hupewa Mhariri pekee, wakati mwandishi naye anahusika kwa njia moja ama nyengine katika huchangia na matumizi mabaya ya lugha ya kiswahili.

Aidha, kutokana nan a Kanuni za Maadili kwa Wanataaluma wa Habari (2016) imegusia suala zima la ubaguzi ambapo imeeleza;-

“Wahariri wahakikishe habari zisiwe na ubaguzi wa jinsia, dini, makundi ya watu wachache, hadhi ya jamii, masuala ya ngono, umri, kabila, rangi, au ulemavu wa aina yoyote ile.

Hata hivyo, pale inapokua muhimu kwa manufaa ya umma, habari hiyo iwe na maoni ya watu”.

Kutokana na matumizi mabaya ya lugha hivi karibuni tumeshuhudia vyombo viwili vya habari vikifungiwa na TCRA, ambavyo ni Clouds Tv pamoja na Wasafi Fm, mbali ya ukiukwaji wa sheria za habari, lakini vituo hivyo vilikuwa chanzo  kikubwa cha kubananga lugha katika baadhi ya vipindi vyao, hiyo ni mifano michache tu.

TCRA kuvifungia vyombo vya habari, kutokakufanya kazi kwa muda, inawezekana ikawa ni jambo jema kwa mujibu wa mamlaka ya TCRA, lakini je kwa upande wa wagombea kutumia lucha zenye kuonyesha chuki na uchochezi tuseme tume ya uchaguzi haina mamlaka ya kuwaonya wagombea hao?.

Kwa mantiki hiyo basi, ipo haja kwa vyama vyote vilivyosimamisha wagombea katika nafasi zote wawe makini katika matumizi ya lugha, kwani matusi, dharau, chuki na uhasama sio kitu cha maana na ustarabu wa taaifa hili.

Lakini pia ifahamike kwamba unapowatukana viongozi wa chama kingeni ndani ya wafuasi wako baadhi yao ni ndugu zao na ni watu wa muhimu sana kwako, je hamuoni kwamba matusi na dharau zitawafanya baadhi ya wapia kura wenu kuwachukia na kuwakosesha kura na kuwapa mnao watukana?

Ifahamike kwamba wanaopiga kura ni wananchi,  tena wenye rika na elimu tafauti sio majuha, wanajuwa lipi jema na baya, hebu wanasiasa wasikilizeni viongozi na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi, yupo mgombea ambaye ametumia lugha zisizo rasmi?

Aidha, lugha ya kiswahili ni tajiri na yenye maneno mengi matamu na mazuri, ambayo yakitumiwa vizuri humvutia msikilizaji.

Kazi na jukumu kubwa la mwandishi wahabari ni kuhakikisha kwamba jamii inaishi kwa amani na sio jukumu lake katika kutukuza uovu, uhalifu au tabia zote mbaya katika jamii na  hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Hivyo basi, uwepo na uhuru wa kila mtu kumiliki ‘Online Tv’ nalo ni tatizo katika matumizi ya lugha, kwani ni dhahiri televisheni za kwenye mitandaoni hazina wahariri kila mtu hufanya atakalo na ndio maana asilimia kubwa za lugha za matusi kwa viongozi zipo kwenye televisheni hizo za mitandao.

Ni jambo la kusikitisha sana, kuona taaluma hii ya habari ambao ni nguzo muhimu katika mihimili ya serikali ikiwa imekumbwa na utata, utashi na uchochozi wa makusudi katika jamii.

Ni vyema waandishi wasiandike au kuonyesha au kutoa maelezo zaidi ya uhalifu kwa namna yoyote ile, ambayo itawashawishi au kuchochea watu kuiga au kufanya majaribio ya matukio hayo.

Kama ambavyo baadhi ya video zinazorushwa kwenye makundi ya ‘whatssap’ au kwenye ‘Online’ zinakwenda kinyume na maadali.

Inawezekana kabisa vyombo vya habari hivyo vya oneline havina wahariri au wapo ila hawana ujuzi wa kuhariri habari zao, kama wapo basi ni vyema wafahamu kuwa jukumu lao la kuhariri habari ni zito na la thamani sana kwao na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, Wahariri hawana budi kujua na kuelewa mambo yaliyomo au kuonyeshwa katika habari, ili kutambua athari zake kwa wasomaji, watazamaji pamoja na wasikilizaji, ingawaje jukumu hili pia linapaswa kufanya na mwandishi mwenyewe kabla habari haijafika kwa mhariri.

Ni wajibu wa vyombo vya habari kwa kupitia kalamu za waandishi wao, kufanya tathimini na uteuzi wa maneno katika kuwasilisha ujumbe wake, matumizi mazuri ya kiswahili,  yanapaswa yafanyike pia kwa viongozi wa  vyama vingine vya kisiasa.

Iwapo hali hiyo itatendeka kwa weledi mkubwa kutastawisha umoja na mshikamano ulipo nchini.

Ni vyema tukafahamu kwamba, Habari au Tangazo lenye taarifa au ujumbe wenye kashfa, dharau, uchochezi au ushawishi wenye nia mbaya ni vyema isichapishwe, kwa maslahi ya umma na jamii kwa ujumla.

Kwa kuwa uchaguzi mkuu ni kielelezo tosha cha utawala bora, hivyo basi matumizi ya lugha jambo la msingi sana katika ustawi wa taifa huru kwa ajili ya kudumisha amani, mshikamano na maendeleo.

Zanzibar mara nyingi ni kituo muhimu cha lugha ya Kiswahili duniani na wengie wao hufika kujifunza na kwenda kufundisha nchini kwao, hivyo ni lazima kuwepo na usimamizi na matumizi bora ya lugha ya Kiswahili.

Kwa kuwa hadi sasa taifa lipo katika amani na utulivu, hivyo ni vyema kukitumia Kiswahili katka kuhakikisha Amani, umoja na upendo kwa maslahi ya wanasiasa na wananchi wa taifa hili kwa ujumla.