ZANZIBAR ni nchi inayojipambanua kwamba ni ya wapenda michezo kutokana na jinsi wananchi wake walivyo na hamasa na ushabiki wa michezo mbalimbali bila ya kuwepo ushawishi wowote.

Kwa mantiki hiyo, ushabiki na mapenzi ya michezo kwa wananchi yapo dhahiri kama ilivyo kwa mataifa mengine ambayo michezo imejengewa misingi bora na yenye kuleta tija badala ya malumbano.

Ni ukweli usiopingika kwamba Zanzibar imejaaliwa kuwa na wanamichezo wenye vipaji na wanaoweza kucheza popote, lakini, kinachokosekana ni usimamizi kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhmana jambo ambalo hivi sasa linahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa ili kupata viongozi watakaokuwa tayari kwa hilo.
Tunasema hivyo kutokana na yale ambayo yamekuwa yakiendelea kwenye vyama vyetu vya michezo kwa kuwepo tofauti za kimakundi ndani ya safu za uongozi, hali ambayo imekuwa ikitajwa kurudisha nyuma maendeleo ya michezo kwa miaka mingi.

Lakini, tukiwa wadau wakubwa wa michezo, tunaamini ikiwa kasoro kama hizo zitafanyiwa kazi kikweli, tunaweza kutoa sura mpya ya michezo Zanzibar na kuwa chachu ya kujikwamua hapa tulipokwama sasa kutokana na sababu mbalimbali.

Hakuna ubishi kuwa kutokana na vipaji vilivyopo katika nchi yetu, endapo tutaendelea kuwekeza zaidi, bila ya shaka tutarajia mambo mazuri mengi katika siku zijazo katika sekta hii ya michezo.
Ni dhahiri kwamba tumekuwa na kiu kubwa ya kupata mafanikio ya michezo sambamba na kuziona timu zetu zikicheza hatua ya juu zaidi ya michuano mbalimbali ya kimataifa kwa mustakabali wa nchi na maendeleo yake kwa ujumla.

Lakini kwa bahati mbaya tumekuwa wanyonge katika hilo huku kukosekana kwa watendaji wakweli kwenye usimamizi wa michezo ukionekana kama kikwazo kifikia huko.

Kutokana na hali ilivyo ni wazi kwamba tunahitaji kujipanga upya tukiwa na mtazamo tofauti na mipango madhubuti ya kurudisha heshima ya michezo katika visiwa hivi.
Lakini ukweli unabakia pale pale kwamba tunahitaji kwenda mbali zaidi huku tukiwa na ujasiri wa kuamini kwamba tunaweza kuvuka kutoka hatua moja na kusogea mbele zaidi ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.

Kinachohitajika hapa kwanza ni kujitathimni na hali tunayoendelea kuizoea ya kuwa watu tuliokosa mipango na kufanya mambo kwa mazoea bila ya kujali gharama ambazo viongozi wetu wa juu wa nchi wanaingia katika kuinua sekta ya michezo kama zilivyo kwa sekta nyengine.

Lakini hapa hatukusudii kumnyooshea kidole yoyote yule, bali ni kuangalia njia za kujitathimni na kuelewa wapi tunakoelekea ikiwa hali ya sasa ya michezo yetu itaendelea hivi ilivyo sasa.

Kwa kipindi kirefu, ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye michuano ya kimataifa haujakuwa mzuri na kumekuwepo na dhana iliyojengeka miongoni mwa mashabiki kwamba sisi ni wa kawaida mno.Hivyo, lazima tufike mahali na kuondokana na dhana hiyo kwa kujitambua kwamba tunahitaji maendeleo ya michezo na hilo litafanikiwa kwa kuleta mageuzi chanya kwa ajili ya taifa.
Zanzibar yenye maendeleo ya michezo inawezekana.