LONDON,UINGEREZA

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea kushtushwa kwake na ripoti kwamba skuli moja kwenye mji wa Kumba kusini magharibi mwa Cameroon ilishambuliwa tarehe 24 mwezi huu na watoto kadhaa kuuawa.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New York ilimnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa katika tukio hilo watoto wengine kadhaa walijeruhiwa.  

Alisema,shambulio hilo la kuchukiza ni kumbusho juu ya gharama kubwa ambayo raia wakiwemo watoto wanalipa huku wakinyimwa haki yao ikiwemo elimu. Mashambulio dhidi ya maeneo ya skuli lazima yakome kwa kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto.”

Guterres alituma salamu zake za rambirambi kwa familia za watoto waliopoteza maisha huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Alitoa wito kwa serikali ya Cameroon ifanye uchunguzi wa kina ili wahusika wa shambulio hilo wafikishwe mbele ya sheria.

Katibu Mkuu pia alitoa wito kwa pande zilizojihami kwa silaha zijizuie kufanya mashambulizi dhidi ya raia na ziheshimu sheria za kimataifa za kibindamu na za haki za binadamu.

Kile kilichoanza kama harakati za raia wa magharibi mwa Cameroon kusaka haki sasa kimegeuka na zimeongezeka na kuwa janga kamili la uasi.

Wazungumzaji wa Kiingereza wanaunda karibu asilimia 20 ya wakaazi wote milioni 20 wa Cameroon, nchi ambayo lugha yake rasmi ni Kifaransa.

Wazungumzaji hao wa Kiingereza katike eneo la magharibi mwa nchi hiyo wanalalamika kuwa wananyanyaswa na kutengwa na serikali kuu na wananyimwa haki zao kama raia wa Cameroon hivyo baadhi ya wakaazi wa eneo hilo walianzisha uasi wakitaka kujitenga.