NAIROBI,KENYA
WZIRI wa Utalii nchini Kenya Najib Balala amesema, nchi hiyo inapanga kutumia umaarufu wa wanariadha wake duniani kuboresha sekta ya utalii.
Katika taarifa yake iliyotolewa jijini Nairobi, Balala alisema, licha ya wanyamapori, ambao ni kivutio kikubwa cha watalii, taswira ya nchi hiyo inatambulika duniani kutokana na kuwa na wanariadha wenye majina makubwa.
Alisema wanariadha hao wameipa Kenya sifa kubwa ya kimataifa kila wanaposhinda, hususan kwenye mbio za marathon.
Kutokana na hilo, Balala alisema wataunda timu itakayoandika taarifa za wanariadha wote nchini Kenya tangu uhuru ili kuwaenzi, na pia kutumia wanariadha hao kutangaza vivutio vya utalii nchini humo.
Balala pia alisema, serikali inataka kutambua, kuendeleza na kutangaza mkoa wa North Rift, ambao ni maskani ya wanariadha maarufu kama kituo cha utalii.