NAIROBI,KENYA

WAZIRI  wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe ameonya kuwa kuna uwezekano nchi hiyo ikakumbwa na maafa kutokana na wananchi,hasa vijana, kupuuza kanuni za kiafya za kuzuia maambukizi ya corona.

Kagwe alitangaza kesi 685 mpya za corona na aliwaonya vijana waache kucheza na ugonjwa hatari wa corona.

Aidha aliwakosoa wanasiasa ambao wanahutubia mikutano ya hadhara ambayo washiriki hawazingatii kanuni za kimsingi za afya za kuzuia corona kama vile kuvaa barakoa na kutokaribiana.

Kagwe amebainisha wasi wasi wake kuwa, wananchi, wakiwemo wahudumu wa afya walianza kurejea katika maisha yao ya kawaida katika hali ambayo janga la corona bado lingalipo.

Waziri wa Afya wa Kenya alisema kiwango cha maambukizi kiliongezeka kwa asilimi 12 kutoka asilimia nne wakati Serikali ilipopunguza zuio la corona.

Kagwe alisema hadi sasa waliopoteza maisha nchini Kenya kutokana na corona ni 832 huku walioambukizwa wakiwa ni zaidi ya 44,000.

Kwingineko, wakaazi wa mji mkuu wa Ufaransa Paris na miji mengine minane waliwekewa marufuku ya kutoka nje kuanzia usiku wa Jumamosi kama hatua ya kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya nchi hiyo kurikodi idadi ya juu ya maambukizi mapya ya watu 32,000 kwa siku moja.

Kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ya virusi hivyo hatari kuliwafanya maofisa nchini humo kuweka hali ya tahadhari nchi nzima.

Wasiwasi wa idadi ya maambukizi kuongezeka umekumba nchi nyingi Duniani.