NAIROBI, Kenya

KOCHA mpya wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, Jacob ‘Ghost’ Mulee ametaja kikosi cha wanasoka atakaowategemea katika mechi mbili zijazo dhidi ya Comoros kuwania kufuzu fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Stars watakuwa wenyeji wa Comoro mnamo Novemba 11 jijini Nairobi, kabla ya kurudiana na Wanavisiwa hao mjini Moroni siku nne baadaye.

 Kati ya wanasoka ambao Mulee amewapa fursa ya kudhihirisha uwezo wao mkubwa uwanjani ni kipa Brian Bwire wa Kariobangi Sharks na Robert Mboya wa Tusker FC.

Daniel Sakari wa Sharks amejumuishwa pamoja na Andrew Juma (Gor Mahia) na Michael Kibwage (Sofapaka) katika orodha ya mabeki watakaotegemewa na Stars.

David ‘Calabar’ Owino wa Zesco United pia amepata fursa ya kudhihirisha ubabe wake kwa mara nyingine katika timu ya taifa.