NEW DELHI, INDIA

MAANDAMANO yamezuka katika sehemu kadhaa nchini India baada ya mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 19 kubakwa na kundi la wanaume na kufariki.

Polisi walisema mwathiriwa kutoka jamii ya Dalit inayoorodheshwa ya chini katika mfumo wa kale wa tabaka nchini India alishambuliwa katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Uttar Pradesh Septemba 14.

Alifariki katika Hospitali moja mjini New Delhi, Polisi waliwakamata wanaume wanne kuhusiana na ubakaji huo.

Wanachama wa jamii ya Dalit mara nyingi huwa waathiriwa wa dhuluma za kingono.

Shirika la Habari la Associated Press linasema msichana mmoja kutoka jamii hiyo mwenye umri wa miaka 13 alibakwa na kuuawa katika jimbo la Uttar Pradesh mwezi Agosti.

Dhuluma za kingono zimeangaziwa nchini India tangu ubakaji wa mwaka wa 2012 uliofanywa na kundi la wanaume kwenye basi dhidi ya mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23 mjini New Delhi.

Alirushwa nje ya basi hilo na kufariki wiki mbili baadaye akiwa kwenye hospitali moja nchini Singapore.

Shambulio hilo lilisababisha kuwekwa kwa adhabu kali dhidi ya wale wanaoshitakiwa kwa uhalifu wa kingono.

Lakini tatizo hilo bado lipo, data za Serikali zinaonesha karibu visa 34,000 vya dhuluma za ngono viliripotiwa mwaka 2018, ikimaanishamwanamke mmoja alishambuliwa kila baada ya dakika 15.