Haijapata kutokea na kama imetokea basi ni sehemu nyengine ya dunia, si Zanzibar kwa serikali kukurupuka kutengeneza sheria isiyo na kichwa wala miguu na kuipeleka kwa wananchi.

Kabla ya serikali kuandaa mswada wa sheria, lazima iwe imefanya utafiti na kubaini tatizo liliopo utatuzi wake unahitaji sheria ili kuzuia, kulinda ama kuhifadhi kitu ambacho kina umuhimu mkubwa kwa maslahi ya jamii.

Jambo jengine muhimu katika kuinasibisha sheria hiyo na jamii, serikali huyashirikisha kikamilifu makundi husika kutoa maoni na michango itakayosaidia kuifanya sheria hiyo iwe bora na kutekelezeka kwa urahisi.

Tunafahamu vyema sheria wanazotunga wanaadamu haziwezi kuacha kuwa na kasoro, kwa sababu mwanadamu mwenyewe ni kiumbe dhaifu na ametolewa kasoro kadhaa na muumba wake.

Sisi hatuna matatizo na sheria zetu zinazotungwa hapa Zanzibar, na tunathubutu kusema kuwa visiwa hivi vimejaaliwa kuwa na sheria nzuri na za kupigiwa mifano.

Sheria tulizonazo zimekuwa nzuri kwa sababu mbalimbali ikiwemo ile ya kufanyiwa utafiti wa tatizo liliopo na ushirikishwaji wa jamii wakati wa kuundwa kwa sheria hizo.

Kitu chengine cha kufurahisha ni kwamba, sheria zetu nyengine zina viwango vya kimataifa na kwamba yale yaliyopo hapa kwetu tuliyoyatungia sheria,   hayana tofauti na nchi za wenzetu.

Pamoja na mazuri hayo, tatizo letu ni utekelezwaji wa sheria hapa Zanzibar, suala hilo limekuwa changamoto kubwa inayoturejesha nyumba na kutofikia maendeleo ya kijamii, kiuchumi wakati mwengine watu hata kupoteza maisha kwa ukaidi tu wa kutofuata sheria.

Labda tutoe mfano mdogo tu tena wa kawaida sana, hivi kuna tatizo gani kwa mtu anayeendesha chombo cha magurudumu mawili kupandia chombo hicho bila ya kuvaa kofia ngumu?