NA ZAINAB ATUPAE

UONGOZI wa klabu ya KMKM,umesema una matarajio makubwa ya kuweka kambi, kujiandaa na ligi kuu ya Zanzibar ya msimu wa mwaka 2020-2021.

Akizungumza na gazeti hili katibu msaidizi wa timu hiyo Suleiman Rajab Mohamed ‘Kisheta’ huko makao makuu wa klabu hiyo Maisara.

Alisema kambi hiyo inatarajiwa kuwekwa Tanzania bara kwenye mikoa ya Morogoro au Arusha, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ambao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Alisema wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki na timu tatu ambazo zinashiriki ligi kuu ya Tanzania.

Alisema hadi sasa wanaendelea kufanya mazungumzo na timu ya Azam endapo wakikubaliana wanaweza kucheza nao,huku wakiendelea kufanya mazungumzo na timu nyengine.

Kwa upande wake ofisa habari wa klabu hiyo Makame Mshenga Makamen alisema timu ipo vizuri na makocha wanaendelea kurekebisha makosa  yaliojitokeza walipocheza na klabu ya Yanga SC hivi karibuni huko Dar es salaam.

“Timu yetu ilicheza vizuri kwenye mechi hiyo,lakini kosa la umaliziaji ndio sababu iliotusababisha tukashindwa kupata mabao,lakini makocha wanayafanyia kazi hasa tatizo la umaliziaji,”alisema.