NA MWAJUMA JUMA
CHAMA cha mpira wa Kikapu Zanzibar (BAZA) kimetangaza majina ya kombiani za Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kwa wanawake na wanaume zitakazoshiriki michuano ya Taifa Cup ya mchezo huo.
Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Mkoani Dodoma Novemba 11 mwaka huu, ambapo timu ya wanaume itakuwa chini ya kocha Barues Ali na kwa wanawake itafundishwa na Amani Kitomari.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Rashid Hamza, alisema wameanza kuchagua kombaini za Unguja na baadae watatangaza na kombaini za Mikoa ya Pemba kwa jinsia zote.
Hata hivyo alisema iwapo kombaini ya Pemba ya wanawake haitopatikana itashiriki kombiaini ya Unguja pekee lakini kwa wanaume inawezekana kushiriki zote mbili.
Aidha alisema kombaini zote hizo zinatarajiwa kufanyiwa mchujo na kupatikana wachezaji 12 kwa kila upande ambao hao ndio watakaokwenda kushiriki michuano hiyo.
Aliwataja wachezaji wanaounda kombaini ya wanawake ni Dawa Abdalla, Sabrina Mohammed, Anameri Cyprian, Sania Khamis (JKU), Helen Simon, Swaumu Haji, Hawa Felecian, Halima Hassan, Mtumwa Khatibu (Zimamoto), Tupegele Lazaro, Boke Juma Regu, Ruth Peter Miwale, Zuwena Nassor, Agness Ayoub Mukasa na Jokha Abdalla (KVZ) na Ummy Abdalla (New West).